Habari MsetoSiasa

Mbunge akana kuambukizwa virusi vya corona

March 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WACHIRA MWANGI

MBUNGE wa Kaloleni, Bw Paul Katana, amekana madai kwamba anaugua na amelazwa hospitalini kutokana na virusi vya corona.

Badala yake, alisema kuwa hali yake ya afya ni nzuri kinyume na vumi zinazoenezwa katika mitandao ya kijamii.

Mbunge huyo alisisitiza kuwa hajawahi kutangamana na Naibu Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Saburi, aliyethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo majuma kadhaa yaliyopita.

“Namshukuru Mungu kwani niko katika hali nzuri kiafya. Siugui na sijalazwa hospitalini kama watu wengi wanavyoamini. Niko nyumbani kwangu na familia yangu,” akasema Bw Katana kwenye mahojiano na Taifa Leo jana.

Alisema kwamba amezingatia kanuni zote zilizotolewa na Wizara ya Afya kuhusu kujitenga kwa siku 14, ikiwa mtu anashuku kuambukizwa virusi hivyo.

Aliongeza kuwa hata amefanyiwa ukaguzi katika Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu (Kemri) katika Kaunti ya Kilifi.

“Niliitwa na kuchunguzwa ambapo ilibainika kwamba sijaambukizwa virusi. Sijui ni kwa nini watu wengi wanasambaza vumi kuhusu hali yangu ya afya. Virusi hivi ni hatari. Ningetaka kuwaonya wale wanaoeneza vumi hizo kupitia mitandao ya kijamii,” akasema.

Aliwaomba Wakenya kuwa waangalifu kwa kuzingatia usafi ili kudhibiti kusambaa kwake.

Alisema kuwa wakati alipokuwa katika mahali palipotengwa, alikuwa akimsaidia mwanawe, ambaye yuko katika Darasa la Nane kudurusu na kusomea nyumbani.

“Wazazi ambao wanao ni watahiniwa wanapaswa kuwasaidia kimasomo katika wakati huu mgumu,” akaongeza.