Kimataifa

Mgonjwa wa kwanza wa corona afariki Tanzania

March 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GAZETI LA THE CITIZEN

MTU wa kwanza Jumanne alifariki nchini Tanzania kutokana na virusi vya corona, ilisema serikali ya taifa hilo.

Akithibitisha kifo hicho, Waziri wa Afya nchini humo, Umy Mwalimu alisema kwamba, marehemu ni mwanamume, na raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 49. Alikuwa akiugua maradhi mengine.

“Ninasikitika kutangaza kwamba tumempoteza mtu kwa kwanza kutokana na virusi vya corona nchini,” akasema.

Mwanamume huyo alifariki katika eneo la Mlongazila, jijini Dar es Salaam.

Alisema kufikia jana, Tanzania ilikuwa imethibitisha visa 19 vya virusi hivyo.

“Kufikia sasa (jana), tumethibitisha visa 19 vya virusi hivyo, ambapo kati yao, mtu mmoja amefariki huku mwingine akitibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini,” akasema waziri huyo.

Tukio hilo linaonekana kuwa pigo kwa Tanzania baada ya mmoja kati ya watu walioambukizwa kupona na kuruhusiwa kuondoka hospitalini mnamo Alhamisi wiki iliyopita.

“Tuna furaha kutangaza kwamba, mtu wa kwanza kati ya wale waliothibitishwa kuugua amepona baada ya kufanyiwa ukaguzi wa kina mara nne. Tuko katika hatua za mwisho kumruhusu kuondoka,” akasema waziri.

Mwanamke huyo, 46, ni raia wa Ubelgiji na alithibitishwa kuambukizwa baada ya kurejea kutoka Ubelgiji mnamo Machi 15 kupitia ndege ya shirika la Rwanda Air.

Mwanamke huyo alibainika kuambukizwa virusi hivyo baada ya kufanyiwa ukaguzi alipowasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro.

Mamlaka za serikali nchini humo zilisema kuwa, mwanamke hakuonyesha dalili zote awali, lakini alianza kuugua akiwa katika chumba alichokuwa amekodisha katika hoteli moja.

Mnamo Jumatatu, Tanzania ilitangaza visa vya watu walioambukizwa virusi hivyo kufikia watu 19, baada ya watu watano zaidi kuthibitishwa kuugua.

Waziri Uma alisema kuwa, kati ya watano hao, wawili wanatoka katika kisiwa cha Zanzibar, huku watatu wakitoka Tanzania bara.“Leo (Jumatatu) tumepokea matokeo kutoka maabara ya kitaifa ya jamii, ambapo watu watano zaidi wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona,” akasema.

Alisema maelezo zaidi kuhusu watu wawili waliotoka Zanzibar yangetolewa na Waziri wa Afya katika kisiwa hicho. Wiki iliyopita, Rais Johh Magufuli alikosolewa na baadhi ya watu alipowaomba Watanzania kutotiwa hofu na maambukizi ya virusi hivyo, badala yake akawaomba kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Hili ni kinyume na nchini Uganda, ambapo Rais Yoweri Museveni Jumatatu alitangaza kufunga shughuli zote za kawaida nchini humo kwa siku 14.