Habari

Corona ni mbio za masafa marefu, watafiti waonya

April 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

JANGA la virusi vya corona ambalo limevuruga sekta zote za maisha litaendelea kwa muda, wataalamu wanaonya na kuwataka Wakenya na serikali kujiandaa kwa nyakati ngumu zaidi.

Wanasema ingawa kufikia sasa watu wanalia maisha yao yamebadilika, ndio mwanzo wa athari za virusi hivyo nchini.

“Hii ni marathoni, jiandaeni binadamu wenzangu. Itachukua miezi kadhaa ya kutotangamana, nakadiria itakuwa miezi minne au mitano,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la utafiti wa matibabu barani Afrika (Amref) Dkt Githinji Gitahi.

“Janga hili sio tukio la muda mfupi la kuruga maisha ya jamii lakini hali hii itachukua muda wa miezi kadhaa kabla ya maisha yetu kurejea hali ya kawaida ya mikutano ya kijamii,” asema Dkt Gitahi.

Kufikia Jumatano, watu 82 walikuwa wameambukizwa virusi vya corona nchini na serikali imebashiri kuwa watu 10,000 watakuwa wameambukizwa kufikia mwisho wa mwezi huu.

Wataalamu nao wanasema hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi miezi ya Mei na Juni huku wakifananisha janga hili na mbio ndefu za marathoni ambazo huhitaji muda na nguvu nyingi.

“Miezi ya Mei na Juni itakuwa kilele cha maambukizi nchini, maelfu ya watu wanatarajiwa kuambukizwa wakati huo iwapo hatua zilizotangazwa za kupunguza kusambaa hazitazingatiwa,” alisema Dkt Gitahi.

Serikali imeweka marufuku ya kutotoka nje usiku, marufuku ya mikutano ya kijamii kama mazishi na ibada na mikutano ya hadhara katika juhudi za kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Kufikia jana, serikali ilikuwa ikifuatilia watu zaidi ya 1000 waliotangamana na waliothibitishwa kuwa na virusi hivi nchini.

Wataalamu wanasema ubashiri wa maafisa wa afya nchini kwamba, watu 10,000 watakuwa wameambukizwa kufikia mwisho wa mwezi huu ni kwa misingi kwamba, wanaofuatiliwa watakuwa wameambukiza zaidi ya watu 10.

Dkt Gitahi aliwataka Wakenya kujiandaa kukabiliana na hali ngumu kwa kukaa nyumbani, kukubali mabadiliko ya mitindo ya maisha ili kuepuka maambukizi.

“Itabidi watu wajifunze kujifungia ndani, kupunguza matumizi ya pesa na kutowekeza katika miradi isiyomuhimu hadi hali itakapobadilika. “Ikiwa mtu alipanga kuanzisha miradi, anafaa kubadilisha nia iwapo mradi huo hausaidii kukabili corona,” alishauri. Wataalamu wanasema uchumi utaendelea kuvurugika serikali ikiwekeza rasilmali zilizotengewa wizara na shughuli tofauti zikitumiwa kukabili janga la corona.

Kulingana na Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe serikali inasimamisha baadhi ya mipango yake ili kupata pesa za kuzuia maambukizi ya virusi hivi hatari.

Dkt Bob Etali, mtafiti wa masuala ya afya na usimamizi anakiri kuwa, hali halisi ya maambukizi ya corona ndio imeanza kubainika Kenya.

“Tunaelekea visa 100 na kulingana na ilivyofanyika katika mataifa mengine ambayo yamekumbwa na janga hili, safari imeisha, tumeanza mbio sasa na zitakuwa na athari kubwa kwa uchumi na mitindo ya maisha ya Wakenya,” asema.

Anabashiri kuwa sekta kadhaa zitapata hasara na watu wengi watapata matatizo ya kisaikolojia.?Mchanguzi wa masuala ya siasa na utawala, Herman Manyora anafanisha janga hili na vita na kushauri serikali kujiandaa kikamilifu.

“Tuko kwa vita na tunahitaji juhudi za pamoja kukabiliana na janga hili,” alisema.