Habari Mseto

Hatimaye Moi aifariji familia ya Matiba

April 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA PETER MBURU

HATIMAYE subira ya Wakenya kwa Rais Mstaafu Daniel Moi kuifariji familia ya marehemu Kenneth Matiba ilivuta heri siku ya Jumatatu, baada ya mwanawe mzee Moi, seneta wa Baringo Gideon Moi kutembelea familia hiyo.

Seneta huyo alifika nyumbani kwa mzee Matiba kufikisha risala za rambirambi, huku ikiaminika kuwa alienda huko kumwakilisha babake Mzee Moi.

Katika picha zilizosambaa mitandaoni, seneta huyo anaonekana akiwa na wanafamilia hiyo wakiwemo mwanawe na mkewe Mzee Matiba na ndani ya nyumba wakizungumza.

Hatua yake hata hivyo, ilikuwa baada ya shinikizo kutoka kwa Wakenya na viongozi kupanda kuwa Mzee Moi aiombe familia ya marehemu msamaha kabla ya mazishi.

Baadhi ya viongozi waliojitokeza wazi kumtaka seneta Moi atembelee familia hiyo ni mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

“Nimekuwa na kazi nyingi hivi majuzi. Kuna uwezekano kuwa nilipitwa na ujumbe wa rambirambi kwa Kenneth Matiba kutoka kwa seneta wa Baringo? Kuna yeyote mwenye habari?” mbunge huyo alichapisha kwenye mtadao wake wa Facebook.

Baada ya ziara ya seneta Moi, Wakenya walimiminika mitandaoni kuelezea hisia zao, huku wengi wakimwondolea lawama kwa makosa yaliyotendeka babake alipokuwa mamlakani.

Hata hivyo, wakenya wengine walihisi kuwa seneta huyo alichukua hatua hiyo ili kujijengea sifa kisiasa.