Habari Mseto

KICD na Safaricom kufunzia watoto nyumbani

April 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

TAASISI ya Kutengeneza Mitaala Kenya (KICD) inapanga kushirikiana kampuni ya Safaricom na wachapishaji vitabu, kuhakikisha kuwa kila Mkenya amepata maelezo kuhusu mpango wa wanafunzi kusomea majumbani mwao kutokana na janga la virusi vya corona.

Tayari, taasisi hiyo imebuni ushirikiano na shirika la KBC, ambalo linapeperusha baadhi ya vipindi vyake kuhusu masomo ya wanafunzi kutoka Gredi 1 hadi Kidato cha Nne.

Kwenye taarifa jana, taasisi ilisema kuwa mpango huo unalenga kuhakikisha kuwa Wakenya wote wanauelewa mfumo huo, ili kuwawezesha wanafunzi kuendelea na masomo yao kama kawaida.

“Mpango huo uko mbioni. Hatua hii inalenga kupanua juhudi ambazo tayari tumeweka kuwafikia wanafunzi popote walipo nchini kupitia vipindi vya masomo,” ikasema kwenye taarifa.

Hatua hiyo inajiri baada ya Mamkaka ya Mawasiliano Kenya (CAK) kuyaagiza mashirika yote yanayotoa huduma za upeperushaji wa matangazo ya runinga kuhakikisha kuwa matangazo ya vituo vya televisheni vya Edu Channel, KBC na idhaa ya KBC yamewafikia wateja wake bila malipo yoyote.

Hapo jana, mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji Kenya (KPA) Bw Lawrence Njagi alisema kuwa mashirika kadhaa ya uchapishaji yamekubaliana kuweka vitabu na vifaa vingine vya kimasomo kwenye tovuti ya KICD ili kuwafaidi wanafunzi katika viwango vyote.

Taasisi vile vile imekuwa ikitoa matangazo ya masomo kupitia tovuti www.kicd.ac.ke na mtandao wa YouTube.

Wiki iliyopita, taasisi ilitoa ratiba maalum ambayo wanafunzi watakuwa wakitumia kufuatilia matangazo ya masomo katika kituo cha Edu Channel kuanzia Jumatatu hadi Jumapili.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wake Dkt Joel Mabonga, aliyashukuru mashirika yote ambayo yamejitokeza kushirikiana nayo, akisema kuwa wanalenga kuupanua hata zaidi.

“Taasisi hii imeendelea kupata uungwaji mkono kutoka wadau mbalimbali katika sekta ya elimu ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaendelea na masomo yao kama kawaida, hata wakiwa majumbani mwao,” akasema.

Wakati huo huo, aliwaomba wazazi kuhakikisha wanao wanafuatilia kwa kina vipindi vya masomo vinavyopeperushwa katika majukwaa mbalimbali.

“Wazazi sasa wanapaswa kuchukua majukumu ya walimu ili kuondoa pengo lolote la kimasomo ambalo huenda likatokea,” akasema.

Kuchipuka kwa virusi hivyo nchini kumepangua ratiba na mipangilio yote ya masomo katika shule za msingi, upili na hata vyuo vikuu kwani haijulikani wakati hali ya kawaida itakaporejea.