• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:58 PM
NGILA: Virusi vimetoa fursa ya kutatua matatizo yetu

NGILA: Virusi vimetoa fursa ya kutatua matatizo yetu

NA FAUSTINE NGILA

HUKU vifo kutokana na virusi vya corona vikiongezeka kila siku, hofu ya maambukizi imetanda kote nchini, licha ya serikali kuweka mikakati ya kuzima gonjwa hili.

Wakenya wengi sasa wameamriwa kufanyia kazi nyumbani, idadi ya abiria kwenye magari ya uchukuzi umma ikapunguzwa, na mikutano ya hadhara ikapigwa marufuku.

Serikali imetangaza kuwa wiki hii huenda tukaingia katika kipindi kigumu zaidi, ambapo kila Mkenya atatakiwa kusalia nyumbani.

Ni kipindi ambacho binafsi nimeshuhudia ongezeko la mauzo ya mitandaoni, na watu wengi wakipendelea malipo ya dijitali.

Hata hivyo, changamoto za watu kutangamana na kubadilishana mawazo ya kufufua uchumi ambao kwa sasa umezama rasmi, bado zipo.

Lakini kwa wapenzi wa teknolojia, huu ndio wakati wa kubuni suluhu ambazo zitasaidia maisha kuendelea.

Baadhi ya wavumbuzi niliosema nao wameahidi kutumia muda huu kubuni majukwaa ya mitandaoni ambayo yataruhusu watu zaidi ya 1,000 kukongamana, ikizingatiwa kuwa makongamano yote ya kimataifa yamesimamishwa.

Programu ya simu ya Zoom, kwa mfano, imepata faida ya matrilioni katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita kutokana na idadi kubwa ya watu duniani wanaotumia huduma za mawasiliano ya video kwa simu.

Ingawa tayari tumeathirika pakubwa, ni wakati wa kuvumbua mbinu za kidijitali kuhakikisha watu wamenunua bidhaa wanazotaka, wamepata riziki na kushiriki ibada.

Kwa mfano, juzi nikimhoji afisa mkuu mtendaji wa maduka ya Tuskys Dan Githua, niligundua kuwa maduka ya jumla pia yamegeukia mifumo ya kuuza bidhaa mitandaoni.

Jumapili, Wakristo wengi hawakufika makanisani kwa ibada. Kwa yakini, gonjwa la corona linawakumbusha watu kuwa unaweza kumfikia Mola bila kwenda kanisani, na kwamba ibada inaweza kupeperushwa moja kwa moja mtandaoni.

Ikilinganishwa na mataifa jirani, Kenya ina bahati kwani ilianza safari yake ya mageuzi ya viwanda awali, lakini suluhu kama M-Pesa, MyDawa, na Uber hazitoshi wakati huu wanafunzi wote wako nyumbani.

Tunahitaji suluhu za mitandao za kuruhusu walimu kuwafundishwa na kuwatahini wanafunzi wangali nyumbani, ili masomo yaendelee kama kawaida. Baadhi ya ripoti zinasema hofu ya corona itapotea tu baada ya miezi 18 kutoka sasa.

Kando na virusi hivi, kuna magonjwa mengine ambayo wanadamu wamekuwa wakiugua. Hapa tunahitaji suluhu za kisasa kuruhusu madaktari kuwapima, kuwapa dawa na kuwapasua wagonjwa kutoka kwa makazi yao.

Tukivumbua baadhi ya suluhu hizi, maisha yetu hayatakuwa magumu kama ilivyo nchini Italia. Tufuate maagizo ya serikali tukifikiria suluhu kwa changamoto hizi.

You can share this post!

NGILA: Tahadhari kuna utapeli wa corona mitandaoni

NGILA: Blockchain itasadia pakubwa kuzima corona

adminleo