• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
ODONGO: Tusisahau nzige, mafuriko tunapokabiliana na virusi

ODONGO: Tusisahau nzige, mafuriko tunapokabiliana na virusi

Na CECIL ODONGO

KENYA ni kati ya mataifa ambayo raia wake wameathiriwa pakubwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Kwa sasa, taifa liko katika hali ya tahadhari huku serikali ikiweka kanuni tofauti za kuzingatiwa na raia kama njia ya kuzuia ueneaji wa virusi hivyo vya maangamizi.

Kati ya mikakati iliyowekwa ni marufuku ya kutotoka nje kuanzia saa moja usiku hadi saa 11 alfajiri na magari ya uchukuzi kuwabeba abiria kwa kiwango cha kadri.

Mengine ni raia kudumisha viwango vya juu vya usafi kwa kunawa mikono wakitumia sabuni.

Napongeza serikali kuu na zile za kaunti kwa kujitahidi kuhakikisha janga hili linatuondokea na kutosababisha vifo jinsi ilivyo Italia, Uhispania, Iran Amerika na mataifa mengine ulimwenguni.

Hata hivyo, ni vyema ifahamike kwamba, vita dhidi ya virusi vya corona haimanishi tusahau kuyakabili majanga mengine yaliyotusibu kabla kisa cha kwanza kuripotiwa nchini.

Nasema hivyo kwa sababu, kwa sasa kuna majanga mawili yaliyofumbiwa macho na hayamakinikiwi ipasavyo.Wengi wanaendelea kuteseka kutokana na uvamizi wa nzige hatari na mafuriko ambayo yameathiri maelfu ya wakazi hasa maeneo ya Nyanza.

Nzige wanaendelea kuvamia mimea mashambani na kuweka taifa katika hatari ya baa la njaa pindi tukapomalizana na janga la virusi vya corona.

Kwa mfano, jamii ya wafugaji katika Kaunti za Samburu, Laikipia, Garissa na Tana River zinalalamika kwamba, wadudu hao wamefyeka kila kitu hali inayosababisha watembee kwa kilomita kadha kutafutia mifugo wao lishe.

Waliotarajia mavuno tele mashambani sasa hawana matumaini tena baada ya nzige kula mimea yao na wengine wadogo kuchipuka baada ya mayai yaliyotagwa awali kuanguliwa.

Cha kusikitisha ni kwamba, Wizara ya Kilimo imekuwa ikijikokota kutoa msaada katika maeneo yaliyoathirika na ilishangaza majuzi kwa kusema bado ilikuwa ikishirikiana na asasi nyingine za serikali kusaidia kupigana na corona.

Je, nzige walikuwa hawatekelezi uharibifu wakati huo?Serikali za kaunti zilizoathirika nazo, zimetelekeza suala hilo na kumakinika kuhakikisha utekelezaji wa mikakati iliyowekwa kuzuia virusi vya corona.

Mafuriko nayo yanaendelea kukumba maeneo tambarare ya Kano eneobunge la Nyando, Kaunti ya Kisumu, Budalangi Busia na Taita Taveta.

Maelfu ya wananchi wanaendelea kukita kambi katika maeneo mbalimbali Kano, baada ya mto Nyando kuvunja kingo zake na maji kusomba mali na makazi yao.

Katika wadi ya Kabonyo Kanyagwal, wananchi wamekita kambi katika kituo cha kibiashara cha Omuonyole na Nyangande huku wengine wakilazimika kuyageuza madarasa ya Shule ya msingi ya Ugwe makazi yao ya muda.

Cha kushangaza ni kwamba, wanasiasa wa eneo hilo, hawaoni mateso na mahangaiko ya watu hawa ila tu virusi vya corona.Kwenye hotuba yake mapema wiki hii, Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o hakutoa ufafanuzi wa kina wa namna jimbo hilo litawasaidia walioathirika na mafuriko hayo.

Aligusia suala hilo kwa maneno machache tu huku wakazi wakilia kaunti imekuwa ikiwahadaa kuwa itawapa msaada.

Kinachosikitisha katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko ni kwamba, kuna hatari ya kutokea kwa mkurupuko wa kipindupindu raia wakikosa vyoo na kutumia maji chafu huku ukosefu wa neti za kukinga mbu ukiwasababishia ugonjwa wa Malaria.

You can share this post!

MUTUA: Corona haiathiri Wazungu tu wengi wanavyofikiria

WANDERI: Yawezekana tunaishi nyakati za mwisho?

adminleo