Habari Mseto

Marufuku yafuta kazi maelfu ya wananchi

April 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na WACHIRA MWANGI

VITUO vya magari ya uchukuzi wa abiria kutoka Nairobi kwenda kaunti za mbali, jana vilisalia mahame kufuatia amri ya serikali ya kutoruhusu watu kuondoka wala kuingia Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale.

Jijini Mombasa, wamiliki wa mabasi walilalama kupata hasara tangu Rais Uhuru Kenyatta atangaze marufuku ya watu kutosafiri kuelekea Nairobi.

Kwenye kituo kikuu cha mabasi ya kwenda Magharibi mwa nchi cha Machakos Country Bus, wahudumu walilalama kuwa wengi watalazimika kukaa bila ajira.

“Amri hii imetukosesha kazi. Kama unavyoona hamna shughuli zozote hapa. Hatujui tutakula nini katika muda wa siku 21 zilizotangazwa na serikali,” akasema Bw Sam Oloo, mhudumu wa mabasi ya Nyaugenya ambayo yanahudumu kati ya Nairobi na Bondo.

Bw Oloo na wenzake walitoa wito kwa serikali ianzishe mpango wa kuwapa chakula watu walioathiriwa na hatua hiyo.

Alisema alifika kituoni hapo kujadiliana na wenzake kuhusu njia mbadala za kujipatia riziki wakati wa marufuku ya sasa.

Mabasi machache ya kampuni za Climax ndiyo yalisalia kuegeshwa katika kituo hicho.

Ni magari mawili pekee aina ya Canter ndiyo wahudumu wake walikuwa wakipakia mizigo ya kwenda Kisii na Kakamega, mwendo wa saa sita mchana.

Wachuuzi ambao kama kawaida hutembeza bidhaa mbalimbali mahala hapo hawakuwepo. Maduka machache na vibanda vya chakula vilikuwa vimefunguliwa.

Uchunguzi wa Taifa Leo katika vituo kadhaa katikati mwa jiji ulionyesha kuwa ni wahudumu wa magari ya kusafirisha mizigo pekee ndio waliokuwa wakiendelea na shughuli zao.

Taswira kama hiyo ilionekana katika eneo la Railways Godown ambako kuna mabasi ya Guardian Angel na Easy Coach.

Vile vile, hapakuwa na shughuli zozote katika barabara za Accra na River Road, ambako kuna vituo vya magari ya kwenda Mombasa.

Jijini Mombasa, wafanyibiashara wa mabasi walisema baadhi ya abiria waliokuwa wamelipa mapema walirejeshewa pesa zao.

Meneja Mkuu wa mabasi ya Mash, Bw Lenox Shallo, alisema walikuwa wameanza kupunguza mabasi tangu kisa cha kwanza cha virusi vya corona kilipotangazwa nchini.

“Sasa tumesimamisha mabasi yote. Tumewapa likizo wafanyikazi wetu hadi tutakapopata tangazo mbadala. Kikubwa ni kuwarejeshea nauli abiria waliokuwa wameshakata tiketi,” akasema Bw Shallo kwenye mahojiano na Taifa Leo.