• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:54 PM
Bei ya bidhaa haijapanda, asema Mkenya nchini Korea Kusini

Bei ya bidhaa haijapanda, asema Mkenya nchini Korea Kusini

Na GEOFFREY ANENE

KOREA Kusini ni mojawapo ya mataifa yaliyoathirika na maambukizi ya virusi hatari vya corona vilivyoanzia katika nchi jirani ya Uchina kabla ya kusambaa katika zaidi ya mataifa 200.

Tovuti ya Taifa Leo ilipata kuzungumza na Mkenya Mercelyne, ambaye ameishi mjini Cheonan kwa miaka mitatu sasa.

Licha ya kuwa Korea Kusini ni jirani ya nchi Uchina na Japan, ambazo pia zimeshuhudia visa vingi vya maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, Mercelyne anasema janga hili limemtia hofu kubwa.

Kabla ya mkurupuko wa virusi vya corona, Mercelyne anasema kutoka mahali hadi kwingine ilikuwa rahisi. Watu walikaribiana na kuendesha shughuli zao bila wasiwasi. Wanafunzi na wafanyakazi walitembea kwa miguu ama kutumia basi ama garimoshi bila hofu.

“Kwa wanafunzi, kufika darasani ilikuwa lazima,” anasema. Hata hivyo, mambo yamebadilishwa na virusi hatari vya corona. “Serikali imepiga marufuku mikusanyiko ya watu na kufunga shule kwa hivyo masomo sasa yanaendeshwa kupitia mitandao ya kijamii.

Wafanyakazi wanaotegemea kazi za ziada walikuwa na ugumu kupata kazi na viwanda vingi vilikuwa vinafanya kazi. Kupata kazi sasa ni ndoto kwa sababu viwanda vidogo vimefungwa. Watu waliotegemea kazi katika viwanda hivyo, sasa wamesalia kukaa nyumbani. 

Bado treni, mabasi na teksi zinafanya shughuli zao kama kawaida, lakini watu wengi wameamua kutumia magari yao binafsi. Wakorea wengi sasa wanafanyia kazi nyumbani. Teknolojia imesaidia sana katika kuandaa mikutano kupitia mitandao badala ya kukutana uso kwa uso.

Watu wengi hapa pia wameamua kununua bidhaa kupitia mitandao na kuletewa hadi katika milango yao badala ya kuenda nje.

Kisa cha kwanza cha virusi hivyo kilipothibitshwa humu nchini, hofu ilituingia kuwa kutakuwa na uhaba wa bidhaa, hasa vyakula. Hata hivyo, serikali ilifanya jambo la maana kudhibiti hali hii na kuondoa hofu kuwa watu watakimbilia madukani kununua kila kitu.

Bei ya bidhaa haijapanda na watu hasa wanaohudumu katika maduka makubwa, masoko, posta na maduka ya kuuza dawa, wanaendelea na shughuli zao.

Tunaendelea na shughuli zetu, lakini pia tukiwa na hofu. Hali ya kiuchumi si nzuri. Watu wengi wanalia hawana fedha kwa hivyo tumelazimika kupunguza matumizi yetu kwa kiwango kikubwa. Inamaanisha kuwa watu wanaofanya biashara za mikahawa ndio wameathirika sana.

Ningependa kushauri Wakenya wenzangu nyumbani wafuate maagizo ya serikali. Kila mtu apatie usafi kipaaumbele. Wale wanaofaa kujitenga wafanye hivyo bila ya kusukumwa.

Kujitenga ni kitu cha maana ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo. Hakuna haja ya kutoka mahali pamoja hadi kwingine bila sababu muhimu. Tafadhalini kaeni nyumbani. Pia, kunyweni maji mengi. Tusaidie serikali na wadau wengine ili waweze kutusaidia. Tudumishe nidhamu.

Naomba serikali pia ifanikishe shughuli ya kupima watu wengi kwa wakati moja. Tufanye kila kitu kinachostahili kufanywa ili tudhibiti maambukizi na kumaliza janga hili. Ni wakati wa kuwa kitu kimoja na kuweka kando tofauti zetu. Pia, tusisahau Mungu. Mungu bariki na kuponya Kenya.”

 

You can share this post!

Hivi ndivyo tunavyoongezea kinga mwilini, asimulia Mkenya...

‘Nilikuja Australia kutazama mbio za magari ya...

adminleo