• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Ndingi alipouza ‘Benz’ yake kununulia watu ardhi

Ndingi alipouza ‘Benz’ yake kununulia watu ardhi

 

Na SAMMY WAWERU

Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Katoliki Raphael Simon Ndingi Mwana a’ Nzeki na ambaye kwa sasa ni marehemu, atakumbukwa kwa mengi aliyotekeleza wakati akihudumu kama Kasisi na Askofu.

Kuanzia viongozi mashuhuri na washirika aliolisha chakula cha kiroho na kutangamana nao, wamemuomboleza kama Mtumishi wa Mungu aliyejawa na roho ya utu.

Askofu Ndingi na ambaye aliaga dunia Machi 31, 2020 akiwa na umri wa miaka 89 baada ya kuugua kwa muda mrefu, ametajwa kama kiongozi wa kidini aliyetetea haki za kibinadamu bila kusahau moyo wake uliojawa na ukwasi hasa kwa kusaidia wasiojiweza katika jamii.

Huku akimiminiwa sifa chungu nzima kutoka kila dira ya nchi na ulimwengu, kuna kitendo kimoja miongoni mwa mengi aliyofanya na ambacho kitasalia kwenye choyo za wengi.

Kwa waliokuwa wakimbizi wa ndani kwa ndani eneo la Molo, kufuatia vita vya kikabila kati ya 1991 – 1992 chini ya utawala wa Rais Mstaafu hayati Daniel Toroitich Arap Moi, wanaishi kumshukuru na kumpongeza marehemu ambaye aliuza gari lake la kifahari, aina ya Mercedes Benz na kutumia mapato hayo kuwanunulia shamba.

Kwa hakika, ni tukio lililogusa wengi, likionesha ukwasi wa utu na ubinadamu aliojawa nao Askofu huyo aliyehudumu hadi kustaafu kwake 2007, na nafasi yake kutwaliwa na Kadinali John Njue.

Akiwa mzaliwa wa lokesheni ya Mwala, Machakos, ambapo alizaliwa mnamo 1931, Askofu Ndingi alitawazwa kuwa Padre 1961, baada ya kupitia mafunzo ya upadre.

Mazishi yake na ambayo yalikuwa ya kipekee, yalifanyika Jumanne, katika kanisa la Katoliki, Holy Family Basilica jijini Nairobi, eneo maalum lililotengewa kuzika maaskofu waliohudumu katika wadhifa wake.

Hafla hiyo iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Katoliki nchini, Kadinali John Njue, ilihudhuriwa na mapadre, makasisi, watawa, wanafamilia na washirika kadhaa, waliokadiriwa kuwa takriban 100 na kuchukua muda usiozidi saa mbili, kufuatia agizo la serikali kutokana na janga la Covid – 19.

Hafla za mazishi zimetakiwa kuendeshwa kwa muda mfupi iwezekanavyo na kuhudhuriwa na watu wachache ili kuzuia maenezi ya virusi hatari vya corona.

Kwenye tawasifu yake iliyosomwa na Padre Lawrence Njoroge, Askofu Ndingi alitajwa kama kiongozi wa kidini aliyebadilisha na kuimarisha maisha ya watu wengi, kote alikohudumu, ndani na nje ya nchi.

“Aliyelala hapa ni SHUJAA, aliyependa kanisa, nchi yake na Wakenya kwa jumla. Wakati wa ghasia za uchaguzi, alitetea wakimbizi wa ndani kwa ndani, na ndio maana 2019 alituzwa na Rais,” Padre Njoroge alieleza.

Kwenye ujumbe wa risala za Rais Uhuru Kenyatta uliosomwa na mmoja wa mhudumu katika afisi yake, Kennedy Kihara, Rais aidha amewataka Wakenya kuiga nyayo za Askofu huyo, akimtaja kama kiongozi wa kidini aliyeipenda nchi yake kwa dhati. “Rais amesema janga la Covid – 19 likiisha, atatenga siku maalum kuongoza taifa kumuomboleza na kumkumbuka Askofu,” Bw Kihara akasema.

Mwili wa Askofu Ndingi na uliowekwa kwenye jeneza la kahawia, juu likichorwa msalaba na maandishi mafupi, ulisitiriwa katika kaburi la maaskofu, lililoko Holy Family Basilica. Aliyekuwa Askofu Mkuu, John Njenga, pia alizikwa katika kanisa hilo.

Aliyekuwa Askofu wa Dayosisi ya Eldoret, marehemu Cornelius Korir pia alizikwa ndani ya Kanisa la Dayosisi hiyo mnamo 2017.

Kabla kuingiza sanduku la Askofu Ndingi katika eneo hilo maalum, Kadinali John Njue, alilitakasa, huku akifuata taratibu za maziko Kikatoliki, akatangulia kumwaga udongo spesheli lilikozikwa, akifuatwa na makasisi na mapadre. Watu wa familia na pia watawa walipata fursa hiyo ya kipekee.

Jaji Mkuu, CJ, David Maraga alikuwa miongoni mwa viongozi wakuu serikalini waliohudhuria mazishi hayo. Wote walioyahudhuria walivalia vitamvua na kuzingatia umbali baina ya mtu na mwenzake.

Buriani Askofu Raphael Simon Ndingi Mwana a’ Nzeki.

You can share this post!

‘Marufuku hii inamaanisha nitalala njaa kwa siku...

Malandilodi Nakuru watisha kung’oa milango kwa...

adminleo