• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:55 AM
Jinsi Kenya inavyoweza kuimarisha viwanda vyake

Jinsi Kenya inavyoweza kuimarisha viwanda vyake

NA SAMMY WAWERU

Kwenye mojawapo ya vitabu vyake, Neglected Value, Roger Wekhomba ambaye ni mtafiti, amechanganua kwa mapana na marefu namna Kenya inavyoweza kuimarika kupitia uboreshaji wa sekta ya viwanda.

Kitabu hicho chenye jumla ya kurasa 131, Wekhomba ametangulia kuorodhesha vigezo muhimu na malighafi yaliyopuuzwa, haswa yakilenga kilimo.

Kwenye simulizi yake, mtafiti huyo anasema ufukara na ukosefu wa kazi hususan kwa vijana, ni masuala yanayoweza kukombolewa ikiwa Kenya itachukua mkondo wa kuboresha viwanda kupitia malighafi ya ndani kwa ndani, badala ya kuyauza nje ya nchi kisha kununua bidhaa zitokanazo nayo.

Wekhomba anahoji, “Kenya ni taifa lenye ukwasi chungu nzima na kuuza malighafi yetu nje ya nchi badala ya kuyaongeza thamani, halafu tunanunua bidhaa kutoka nje, ni sawa na kubunia mataifa hayo kazi”. “Nchi hii tutaikomboa kwa kutambua na kuthamini sekta ya viwanda, ambayo itatuletea utajiri na kubuni nafasi za ajira.

“Huwa tunazungumza jinsi Kenya ilikuwa katika daraja moja na Malaysia, Korea na Singapore mnamo 1968. Tunakosa kubaini mikakati iliyowekwa kuimarisha nchi hizo,” Wekhomba anaeleza kwenye kitabu chake.

Aidha, katika mataifa hayo sekta ya viwanda imepewa kipau mbele, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa teknolojia. Kinachosababisha Kenya kuendelea kusalia nyuma, ni donda ndugu la ufisadi linalosakatwa na viongozi wenye tamaaa ya ubinafsi.

Kwa kiasi kikuu, viongozi tunaochagua na kuteua wanalaumiwa kuchangia masaibu tunayopitia kama taifa lililojaaliwa, kwa kujishughulikia wao wenyewe na kuendeleza ufisadi. Roger Wekhomba anasema, “taifa litaafikia matakwa na maendeleo iwapo tutachagua viongozi wenye maono kutuongoza na kukumbatia uboreshaji wa viwanda”.

Akieleza kuhusu utajiri tulionao, kwa mukhtadha wa Almasi, anasema nishani hiyo kabla kutolewa ardhini haina thamani wala umuhimu wowote, hadi pale itakapochimbwa, isafishwe na kuingia sokoni.

Wekhomba ni mwenye masikitiko tele anapoona mazao ya kilimo yakitupwa kiholela, mengine yakioza na kuishia kutupwa kwa kuwa hayawezi kulika.

Anapofanya ziara kwenye masoko mbalimbali, kinachomuuma zaidi ni kuona maembe, maparachichi, mapapai, machungwa, ndizi, nyanya, miongoni mwa mazao mengine yaliyotupwa na kuchakaa kwenye majaa.

Kabla kufikia kiwango hicho, huwa katika hali shwari lakini kwa sababu ya ukosefu wa soko, wafanyabiashara wanalazimika kuyatupa. Pia, kuna mazao mengine yanayooza kwa sababu ya ukosefu wa njia bora kuyahifadhi.

Hali hiyo inawiana na taswira ya mashambani, ambapo wakulima hukadiria hasara bin hasara kwa ajili ya ukosefu wa soko. Kadhalika, mawakala wanatajwa kuchangia hilo kwa kununua bidhaa kwa bei duni.

Kwa Rodger, hayo yote yanaweza kuepukika. Anapotazama matunda na bidhaa za kilimo zilizotupwa na zingine kuoza, mjasirimali huyo anaona dhahabu.

Anashangaa ni kwa jinsi gani taifa linashuhudia ukosefu wa kazi hasa miongoni mwa vijana, ilhali mazao hayo ni malighafi kuanzisha viwanda. “Kiwanda si majengo makubwa na mashine za bei ghali. Ukiwa na sufuria, kijiko, mwiko, kichujio, vifaa vingine vinavyotumika jikoni na kiini cha moto basi una kiwanda,” Rodger anaeleza.

Mtafiti huyo ni mkufunzi wa uongezaji thamani mazao ya kilimo, ambapo hutumia matunda mbalimbali na mazaohai kuunda mafuta ya kujipodoa, sabuni na viungo vya kuongeza mlo ladha kama vile ‘tomato paste na sauce’, miongoni mwa bihaa zingine.

“Kwa mfano, maparachichi maarufu kama avocado, huyatumia kutengeneza sabuni isiyo na kemikali yoyote,” afafanua.

Matunda kama haya yaliyotupwa baada ya kukosa wanunuzi ni dhahabu kwake. Anahimiza serikali kufanya hamasa uongezaji thamani kwa mazao ya kilimo. Ni mojawapo ya njia kuimarisha sekta ya viwanda nchini. Picha zote/ Sammy Waweru

Nyanya huzitumia kutengeneza viungo, na anasema kinachomkereketa maini ni kuona zikiozea shambani na kwenye masoko. Akitoa mfano wa kisa alichoshuhudia mwaka uliopita, 2019, kwenye soko moja eneo la Athi River, Roger anasema mfanyabiashara mmoja alikadiria hasara ya kreti tatu za nyanya alizodai zimeoza kwa kukosa wanunuzi.

“Nilimpa Sh100 nikazichukua. Hazikuwa zimeharibika alivyosema. Aidha, nilizitumia kama mtihani kutengeneza kiungo kitokanacho na nyanya, tomato sauce,” asimulia.

Anasema nyanya hizo alipoziongeza thamani, kwa muda wa kuku kumeza punje za mahindi alitia kibindoni jumla ya mapato ya Sh12, 000.

Mojawapo ya vifaa vya jikoni anavyotumia kuongeza mazao ya kilimo thamani. Kuanzisha viwanda kulingana naye hakuhitaji maelfu ya pesa.

“Gharama ilikuwa kununua nyanya, maji, kupakia na kuweka lebo. Hebu tathmini hapa, iwapo kila kreti ningeuziwa Sh2, 000, bado ningepata faida ya kuridhisha ya Sh6, 000,” anasema.

Ni hali inayoshuhudiwa katika masoko mengi nchini, wafanyabiashara na wakulima wakiishia kukadiria hasara isiyomithilika. Nyanya, matunda, viazi na mboga zikiwa katika orodha ya mazao yaliyoathirika pakubwa.

“Wakulima na wafanyabiashara wahamasishwe umuhimu wa kuongeza mazao thamani. Hivyo ndivyo viwanda huibuka,” ashauri Steven Mwanzia, mkulima wa matunda na pia mtaalamu wa masuala ya kilimo.

Mwanzia ambaye hukuza matunda aina ya bukini katika Kaunti ya Kiambu, huyaongeza thamani kwa kuunda sharubati na mvinyo. “Matunda tunayolima huyatumia kuunda juisi, mvinyo na divai,” adokeza.

Baadhi ya sabuni alizotengeneza kwa malighafi na mazao ya kilimo, yakiwamo matunda kama vile maparachichi.

Kulingana na maelezo ya Rodger Wekhomba ambaye huendeshea utafiti na gange ya uongezaji thamani mazao ya kilimo eneo la Kiambu, inachopaswa kufanya serikali ni kutilia mkazo suala la uimarishaji na uboreshaji viwanda.

“Maendeleo si ujenzi wa barabara, ila ni kuona kila raia ana kiini cha mapato. Mataifa yaliyoimarika na kukua kiuchumi ni yanayotilia mkazo uimarishaji wa viwanda. Serikali ielekeze mgao mkubwa katika sekta ya viwanda. Mazao ya kilimo pekee yanatosha kutatua suala la ukosefu wa kazi kwa vijana kupitia viwanda vya uongezaji thamani,” Rodger afafanua, akiongeza kuwa hilo linahitaji hamasa kupitia serikali na wadau husika.

Aliingilia shughuli za kuongeza mazao ya kilimo thamani mnamo 2010, na kufikia sasa ana karakana yenye kiwanda cha kazi hiyo. Amebuni nafasi za vijana kadhaa, bila kusahau bidhaa zake pia ziko sokoni, hatua anayoisifia akisema wauzaji wameweza kujiajiri.

Mwaka 1968 Kenya ilikuwa katika daraja moja na nchi kama vile Korea, Malaysia na Singapore. Mataifa hayo kupitia uongozi bora yamepiga hatua nyingi mbele, ambapo sekta ya viwanda imepewa kipau mbele, yote hayo akiyaangazia kwenye kitabu chake ‘Neglected Value’ akiyalinganisha na Kenya.

Hata ingawa amefanikisha azma yake, anasema changamoto inayozingira sekta ya viwanda nchini ni wanunuzi haswa wenye maduka ya kijumla kukosa kuthamini bidhaa za ndani kwa ndani. Anahimizia serikali kubuni sheria zitakazopiga jeki bidhaa zilizotengenezewa humu nchini, kama vile sokoni ziwakilishe asilimia 60.

Kwenye kitabu chake, ‘Neglected Value’, Rodger anasema Kenya ina utajiri wa kutosha kuanzisha viwanda chungu nzima, ila muongozo na hamasa, ni vigezo vinavyokosa. Mazingira duni ya biashara, mtafiti huyo anataja kama vizingiti vinavyochangia wawekezaji wa ndani kwa ndani kuhofia kuwekeza utajiri wao kwenye viwanda.

Kupitia kitabu chake, Neglected Value, ameipa serikali mwongozo wa vigezo inavyopaswa kuzingatia ili kuboresha sekta ya viwanda.

Akicharura viongozi, anasema wanajishughulisha kusambaza utajiri wenyewe kwa wenyewe. “Serikali itathmini namna ya kubuni utajiri kupitia uboreshaji wa viwanda, ambavyo vitabuni nafasi za ajira. Iweke mikakati kabambe kuimarisha utendakazi wake,” amenukuu kwenye kitabu hicho.

Pia, anaendelea kupendekeza ugatuzi utumike kufanikisha sekta ya viwanda, kupitia mgao wa fedha ambazo serikali za kaunti hupokea kila mwaka wa fedha.

You can share this post!

KAFYU: Familia zadai haki baada ya kujeruhiwa na polisi

Bei za bidhaa kupanda zaidi licha ya serikali kuahidi afueni

adminleo