Majaji na wabunge wote kupimwa virusi vya corona
Na VALENTINE OBARA
WABUNGE na majaji wote watachunguzwa kimatibabu hivi karibuni ili kubainisha kama wameambukizwa virusi vya corona.
Waziri Msaidizi wa Afya Mercy Mwangangi, Jumatano alisema serikali itaanza shughuli ya kuchunguza wananchi kwa wingi kuanzia katika asasi kuu za serikali.
Alisema hayo jana alipotangaza kuongezeka kwa idadi ya walioambukizwa virusi hivyo nchini hadi 179.
“Tutakapoanza shughuli hiyo idadi ya walioambukizwa itabainika ni kubwa na tutaona hali halisi ilivyo,” akasema kwenye hotuba ya kila siku ya serikali kuhusu janga la corona.
Serikali ilikuwa imetabiri awali kuwa idadi ya maambukizi itafika 10,000 kufikia mwisho wa mwezi huu.
Kuhusu ripoti kwamba kuna wabunge 17 waliothibitishwa kuambukizwa, Dkt Mwangangi alisema serikali haijapokea ripoti hizo rasmi.
Alitaka hospitali na maabara zilizoruhusiwa katika kutoa huduma za corona, ziwe zikiwasilisha ripoti zao kwa serikali kuu na zisitangaze matokeo kiholela kwa umma.
Waziri huyo msaidizi alifichua kwamba idadi kubwa ya wale walio na virusi vya corona kwa sasa ni walio na nguvu za kufanya kazi. Hii ni kutokana na kuwa kati ya watu walioambukizwa, 114 ni wenye umri wa kati ya miaka 30 hadi 59.
Alisema kuwa ni watoto watatu pekee wa umri chini ya miaka 15 waliopatikana kuambukizwa virusi hivyo kwa sasa.
Wagonjwa walio na zaidi ya umri wa miaka 60 ni 13, huku wenye miaka 16 hadi 29 wakiwa 49. Jana, idadi ya maambukizi mapya ilikuwa saba kutoka kwa watu 305 waliochunguzwa.
Wote saba ni Wakenya. Mmoja alikuwa amesafiri kutoka Congo DRC, mwingine kutoka Uingereza na wawili kutoka Amerika.
Watano walipatikana Nairobi, mmoja Uasin Gishu na mwingine Mombasa. Kati yao, wanne ni wanawake na watatu wanaume.
Wakati huo huo, serikali iliagiza vinyozi wote na wasusi wavae maski wanapohudumia wateja wao.