Padre aliyehatarisha maisha ya watu Siaya akamatwa
Na PHILIP MUYANGA
POLISI jijini Nairobi, Alhamisi walimkamata Padre Richard Oduor punde baada ya kuachiliwa kutoka hospitali ya Kenyatta, ambako alikuwa ametengwa kwa lazima.
Padre Oduor alikuwa ameripotiwa kutangamana na zaidi ya watu 130 katika kaunti za Siaya na Kisumu mwezi uliopita baada ya kurudi nchini kutoka Italia, badala ya kujitenga kama ilivyoagizwa na serikali katika kanuni zake za kukabili virusi vya corona
Kamanda wa Polisi eneo la Nairobi Philip Ndolo alithibitisha kukamatwa kwa padre huyo.
Jijini Mombasa, Naibu Gavana wa Kilifi Gideon Saburi alishtakiwa jana kwa kutangamana na watu akiwa anaugua virusi vya corona bila kuchukua tahadhari.
Bw Saburi, aliyefikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Mombasa Ritah Amwayi, alikanusha shtaka hilo analodaiwa kulitenda kati ya Machi 6 na 22 katika Kaunti ya Kilifi.
Bw Saburi ataendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Port akingoja kusikizwa kwa ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma la kutaka anyimwe dhamana.
Kupitia wakili George Kithi, Bw Saburi aliiambia mahakama kuwa DPP hana uwezo wa kumshtaki chini ya sheria za afya ya umma.
Bw Kithi alieleza korti kuwa afisa wa afya ndiye anayeweza kumshtaki chini ya sheria ya afya ya umma na wala sio DPP.
Kesi hiyo itatajwa Aprili 15, siku ambayo ombi la upande wa mashtaka la kutaka Bw Saburi kunyimwa dhamana na kuwekwa kizuizini peke yake hadi kesi kukamilika litasikizwa.
Kabla ya Bw Saburi kushtakiwa, mahakama ilitupilia mbali ombi la upande wa mashtaka la kutaka azuiliwe katika Gereza la Manyani ili kuwapa polisi muda wa kukamilisha uchunguzi.
Bi Amwayi alisema kuwa kumzuia Bw Saburi kutakuwa ni kukiuka haki zake, kwa kuwa upande wa mashtaka haukutoa stakabadhi za kuonyesha kuwa ni mgonjwa.
Hakimu Amwayi aliongeza kuwa chini ya sheria ya afya ya umma, magereza hayakutarajiwa kuwa mahali pa kutenga watu wagonjwa kwa kuwa hiyo inahatarisha afya ya wale walioko gerezani.
Korti pia ilisema hakukuwa na ushahidi kuwa Bw Saburi alikuwa amesafiri Ujerumani, na iwapo nchi ilikuwa imetajwa kama nchi ya tahadhari kubwa.