Kiungo wa Bandari 'Messi' asajiliwa Belarus
Na CHRIS ADUNGO
KIUNGO matata wa Bandari FC, Mohammed ‘Messi Agege’ Katana, ameingia katika sajili rasmi ya kikosi cha FC Smolevichi nchini Belarus.
Ingawa Bandari wamethibitisha uhamisho wake, kikosi hicho kutoka Pwani ya Kenya hakijafichua urefu wa muda ambao Katana atakuwa akipiga soka ndani ya jezi za Smolevichi.
“Katana ni mchezaji wa haiba kubwa. Imenishangaza kwamba imemchukua muda mrefu kiasi kupata kikosi cha kujivunia maarifa yake ughaibuni. Ana utajiri mkubwa wa kipaji na ghera ya kutaka ushindi katika kila mchuano,” akatanguliza meneja wa Bandari, Wilson Oburu.
“Cha kusikitisha tu ni kwamba hajapata majukwaa mwafaka zaidi ya kudhihirisha ukubwa wa uwezo alionao katika mashindano mbalimbali ya soka ya humu nchini,” akaongeza Oburu ambaye ni kipa wa zamani wa Harambee Stars.
Katana alianza taaluma yake ya soka katika akademia ya Aspire alikofunga mabao mawili dhidi ya Real Madrid na kuongoza kikosi hicho kutwaa ubingwa wa Kass International Tournament mnamo 2018.
Alijiunga na Bandari kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu mnamo Septemba 2019 baada ya kukatiza uhusiano wake na kikosi cha Leixoes SC nchini Ureno. Katika kibarua chake cha kwanza chini ya kocha Bernard Mwalala kambini mwa Bandari, alifunga bao dhidi ya Zoo Kericho mnamo Septemba 2019.
Alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Harambee Stars cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mnamo 2018.
Kikosi cha Smolevichi kilichoasisiwa mnamo 2009, kilianza kushiriki Ligi ya Daraja la Pili nchini Belarus mnamo 2010 na kupandishwa ngazi hadi Ligi Kuu mnamo 2012. Tangu 2016, wengi wa wachezaji wa Smolevichi wamekuwa wakitokea katika akademia ya klabu ya BATE Borisov nchini Belarus.
Smolevichi huchezea mechi zao za nyumbani katika uwanja wa Stadyen FLC Oktyabrsky ulio na uwezo wa kubeba mashabiki 1,000 pekee. Hadi Ligi Kuu ya Belarus ilipoahirishwa kutokana na virusi vya corona, Smolevichi walikuwa wakishikilia nafasi ya 12 jedwalini kwa alama moja baada ya mechi mbili za ufunguzi wa msimu huu.