Habari Mseto

Uzoaji vifaa vya corona wazua hofu

April 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MISHI GONGO

FAMILIA zinazoishi katika eneo la Mwakirunge mjini Mombasa zinahofia kuambukizwa virusi hatari vya corona kufuatia kutupwa kwa glavu na barakoa zilizotumika katika eneo hilo.

Mnamo Ijumaa, Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe alitangaza kuwa wizara yake, Shirika la Kusimamia Mazingira Kitaifa (NEMA), na Wizara ya Mazingira zilikuwa zishawasilisha mwongozo kwa serikali za kaunti kuhusu jinsi ya kuharibu barakoa na glavu zilizotumiwa.

Wiki iliyopita, NEMA ilisema vifaa hivyo vinafaa kuchukuliwa kama vifaa vya kimatibabu kwa hivyo havifai kutupwa kiholela bali kukusanywa mahali pamoja na kuchomwa.

Familia za Mwakirunge ambazo makazi yao yamezungukwa na jaa kubwa la taka wanaishi kwa wasiwasi kwani bidhaa zinazoaminika kutumiwa hospitalini zinatupwa katika jaa hilo na kuhatarisha maisha yao.

Akizungumza mnamo Ijumaa, Bi Tabu Kadege ambaye ni mkazi wa eneo hilo alisema, familia nyingi katika eneo hilo zinategemea jaa hilo katika kuchuja baadhi ya bidhaa zinazotupwa hapo kama vile chupa za plastiki na vyuma vikuukuu wanavyouza ili kujipa pato lao la kila siku.

“Tunaomba serikali ya kaunti hii kuhakikisha vitu ambavyo vinaweza kusambaza virusi hivyo havitupwi katika eneo hili. Watoto na wanawake hutegemea vipuri katika jaa hilo kujipa riziki,” akasema.

Aidha, alisema watoto wao hucheza katika eneo hilo, hivyo kuwaweka katika hatari ya kuambukizwa iwapo vifaa hivyo vitakuwa na viini vya corona.

Mkazi mwengine, Bw Munga Mtanje alisema, kufikia sasa hawajapokea hamasisho wala vifaa vyovyote vya kujikinga na kuzuia maambukizi hayo kutoka kwa serikali. “Glavu na vitamvua vinavyotupwa eneo hili hatujui hali ya kiafya ya watu waliovitumia. Watoto wetu hucheza eneo hilo, iwapo vifaa hivyo vina virusi basi eneo hili litaathirika pakubwa,” akasema.

Bw Mtanje alisema suala la kuosha mikono kwa sabuni kila mara linasalia kuwa ndoto kufuatia uhaba wa maji katika eneo hilo na bei za juu sabuni inayofaa.

Bw Mtanje alisema wakazi wanalazimika kutembea masafa marefu kupata maji ya matumizi. Ziara ya gazeti la Taifa katika eneo hilo ilibaini kuwa wakazi katika eneo hilo hawafuati kanuni zilizowekwa na wizara ya afya .

Wakazi hao waliendeleza shughuli zao za kuchakura jaa bila glavu wala vitamvua. Aidha hawazingatii amri ya watu kutokusanyika katika eneo moja.

bila kupeana umbali wa mita moja.

Kulingana na Nolly Wilson kutoka shirika la KUZA na vile vile mwenyekiti wa mtandao wa mashirika yanayoshughulikia haki za watoto hapa Mombasa, eneo hilo linahitaji hatua za dharura ili kukabili changamoto zinazoshuhudiwa na wenyeji wa eneo hilo haswa katika kukabili virusi vya corona.

Kauli yake iliungwa mkono na Rehema Natasha kutoka kituo cha makao ya watoto cha Wema akipendekeza serikali ya kaunti na wahisani kuwasilisha msaada wa dharura eneo hilo kwa kuhakikisha kuna maji kila wakati pamoja na vifaa vingine sawa na kuhakikisha maafisa wa afya ya umma wanatumwa eneo hilo kutoa hamasisho kuhusiana na kujikinga na maambukizi hayo.

“Tunaomba maafisa wa afya ya Umma kutembelea eneo hili,kuhamasisha wakazi kuhusiana na virusi vya corona,” akasema.