Ishara huenda Bundesliga ikarejelewa
Na CHRIS ADUNGO
SIKU chache baada ya Bayern Munich kurejelea mazoezi, kikosi cha Eintracht Frankfurt ambacho pia kinashiriki Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kimefuata mkondo.
Kwa mujibu wa kiungo Gelson Fernandes wa Frankfurt na timu ya taifa ya Uswizi, kurejea kwao kambini kwa minajili ya mazoezi ni dalili zinazoashiria uwezekano wa kipute cha Bundesliga kuanza upya kufikia mwisho wa Mei 2020.
Timu za Ligi Kuu ya Ujerumani ndizo za kwanza katika soka ya bara Ulaya kurejea mazoezini baada ya virusi vya homa kali ya corona kusitisha shughuli zote za michezo duniani kote.
Bundesliga ilisimamishwa kwa muda mnamo Machi 13 na hakuna ishara kwa itarejelewa mnamo Aprili 30 kama ilivyoratibiwa hapo awali.
“Bundesliga itakaporejelewa, nadhani wachezaji wataruhusiwa kuchezea ndani ya viwanja vitupu bila mashabiki. Ilivyo, dalili za kuanza upya kwa kipute hicho mwishoni mwa Mei zipo.
Kuwazia Juni, Julai na Agosti ni kwenda mbali sana. Hata hivyo, sioni uwezekano wowote wa kucheza mbele ya mashabiki 50,000 kabla ya Septemba 2020,” akasema Fernandes ambaye ni mchezaji wa zamani wa Manchester City.
Kwa mujibu wa Fernandes, 33, wachezaji wanne wa Frankfurt waliwahi kuthibitishwa kuambukizwa virusi vya corona na wakatengwa kwa kipindi cha siku nne kabla ya kutibiwa na kupona.
Sawa na hali ilivyo kambini mwa Bayern, wachezaji wa Frankfurt pia hushiriki mazoezi katika makundi ya masogora watatu au wanne na hawatakiwi kutagusana kwa karibu sana huku msisitizo zaidi katika mazoezi yao ukiwa ni kupiga pasi na kulenga shabaha.
Ni wachezaji watatu pekee ndio wanaokubaliwa katika chumba cha kubadilishia sare kwa wakati mmoja.
Katika mahojiano yake na gazeti la New York Times, Afisa Mkuu Mtendaji wa Bundesliga, Christian Seifert, amesema kwamba wanabuni mipango na mikakati itakayoshuhudia Ligi Kuu ya Ujerumani ikirejelewa kufikia katikati ya Mei huku kwa matarajio kwamba mechi tisa za mwisho wa msimu huu zitakuwa zimesakatwa kufikia mwisho wa Juni 2020.
Mbali na Frankfurt, klabu nyinginezo za Bundesliga ambazo zimeshuhudia wachezaji wao wakipunguziwa mshahara kwa hadi asilimia 20 kutokana na virusi vya corona ni Bayern, Borussia Dortmund na Union Berlin ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 11 jedwalini.
Katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), vikosi ambavyo vimeshuhudia wachezaji wakikatwa mshahara katika juhudi za kukabiliana na janga la corona ni Southampton na West Ham United pekee.