Habari Mseto

Ninunuliwe wali kwa nyama, sipendi kabeji, mshukiwa amlilia hakimu

April 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na Richard Munguti

MSHUKIWA wa wizi wa mabavu aliomba mahakama iamuru anunuliwe chakula na maafisa wa polisi waliomfikisha kortini kwa vile anahofia atakufa njaa akiwa runande.

“Mheshimiwa tumbo langu limeshikana na mgongo kwa sababu ya njaa,”Carlos Nzioka Wambua alimweleza hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bi Martha Nanzushi.

“Sababu gani tumbo lako limeshikana na mgongo?” akauliza Bi Nanzushi.

Akijibu alisema: “Tangu tuliposhikwa Aprili 9 2020 na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Central tunalishwa kwa kebeji na mimi huwa sili mboga hiyo kwa sababu ya kuchafuka tumbo. Kila siku nimekuwa nikipewa tosti mbili na chai kila asubuhi. Mkate na chai ndio nategemea kwa maankuli yangu. Nimeteseka kwa kukosa mlo.”

Kutoka kulia waliosimama: Carlos Nzioka Wambua almaarufu Peter Kimani Njenga, Paul Muinde Mutua na Dennis Munguti Mutuku wakiwa kizimbani kwa shtaka la wizi wa mabavu. Picha/ Richard Munguti

Carlos aliomba korti iamuru anunuliwe chakula kama vile wali kwa nyama ama chapati kwa karanga ama ndengu.

Hakimu aliwaamuru kiongozi wa mashtaka Abel Amareba na afisa anayechunguza kesi hiyo wamnunulie mshtakiwa chakula ale ashibe kabla ya kurudishwa seli.

Pamoja na Paul Muinde Mutua na Dennis Munguti Mutuku waliachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 kila mmoja baada ya kukamusha shtaka la kumnyang’anya Stephen Sang Kipng’eno simu yenye thamani ya Sh3,500.

Walikuwa wamejihami kwa kisu walipomvamia Kipng’eno Aprili 9 katika bustani ya Uhuru mwendo wa saa sita unusu.

Kesi itatajwa Aprili 30.