50 waliohepa karantini Nairobi wasakwa
BENSON MATHEKA Na PIUS MAUNDU
SERIKALI inachunguza ripoti kuwa watu 50 waliokuwa wamewekwa karantini katika chuo cha mafunzo ya utabibu jijini Nairobi (KMTC) kwa kukiuka amri ya kutotoka nje usiku, walitoroka katika hali isiyoeleweka mnamo Jumatatu jioni.
Waziri msaidizi wa Afya, Dkt Mercy Mwangangi alisema kwamba wizara hiyo ilipata habari hizo na ikaagiza wizara ya usalama wa ndani kufanya uchunguzi.
“Ni kweli tumeona habari katika mitandao ya kijamii kuhusu kutoroka kwa watu waliokuwa karantini katika chuo cha KMTC na tumeagiza uchunguzi kubaini hasa kilichotendeka. Tunasubiri ripoti ya uchunguzi huo kabla ya kutoa taarifa kamili,” alisema Dkt Mwangangi alipokuwa akitoa taarifa ya kila siku kuhusu hali ya virusi vya corona nchini.
Duru zilisema kwamba watu hao walikuwa wakilalamika kuwa hawangemudu gharama ya Sh2,000 kila siku ambayo wanaowekwa karantini kwa kukiuka kafyu wanatakiwa kulipa.
Waziri wa Afya, Be Mutahi Kagwe alisema kwamba watu hao watawekwa karantini kwa gharama yao wenyewe.
Kutoroka kwao kunajiri huku serikali ikisema maambukizi yanaendelea kuongezeka nchini. Jana, Dkt Mwangangi alisema idadi ya waliothibitishwa kuwa na virusi hivyo nchini imefikia 296 baada ya visa vipya 15 kuthibitishwa. Saba ya visa hivyo vilithibitishwa katika Kaunti ya Mombasa,
Sita vilithibitishwa katika Kaunti ya Nairobi na mbili Kaunti ya Mandera. Wiki jana, watu 32 walitoroka kutoka karantini ya Mandera na baada ya uchunguzi serikali ilisema waliwahonga maafisa wa usalama ili waweze kuhepa.
Mnamo Ijumaa, Bw Kagwe alisema kuwa watu 455 walikuwa wamezuiliwa karantini kwa kukiuka amri ya kutotoka nje usiku. Alisisitiza kuwa watakaopatikana nje wakati wa kafyu watachukuliwa kuwa waliotangamana na watu walio na virusi na watatengwa kwa siku 14.
Katika Kaunti ya Makueni, watu 37 wakiwemo makahaba 30 na wateja wao waliwekwa karantini kwa kukiuka kafyu.
Dkt Mwangangi alisema wizara ya Afya inatayarisha mwongozo ambao maafisa wa polisi watakuwa wakifuata wakiwakamata washukiwa wakati huu wa janga la corona.
Hii ni baada ya kuibuka kuwa baadhi ya maafisa hao wamekuwa wakiwakamata washukiwa hao bila kufunika mdomo na pua kwa barakoa na kuwabeba wakiwa wamerundikana katika magari.
Katika Kaunti ya Makueni, wanawake 30 wanaoshukiwa kuwa makahaba ni miongoni mwa watu 37 waliotengwa kwa siku 14 katika shule mbili za sekondari.
“Tuliwakamata wanawake 14 waliovalia mavazi yaliyoacha sehemu za mwili zikiwa wazi katika chumba cha wageni cha Kilungu Lodge. Katika Under 18 Lodge, tuliwakamata wanawake makahaba 10 na wateja wao sita,” alisema mkuu wa polisi eneo la Nzaui, Bw Josiah Dullo.
Wahudumu wawili wa baa pia walikamatwa wakiuza pombe pamoja na wateja wao wawili. Watu watatu walipatikana wakizurura nje saa za kafyu.
Watu hao 37 walipelekwa kituo cha polisi cha Emali kabla ya kuhamishiwa vituo vya kutenga wanaoshukiwa kuwa na virusi vya corona katika shule ya upili ya Mulala Girls na ya wavulana ya Matiliku.
Kamishna wa kaunti hiyo, Bw Mohammed Maalim mnamo Jumatatu aliagiza machifu na manaibu wao kuwakamata watu wataopatikana bila barakoa katika maeneo ya umma.