Habari Mseto

Kampuni za ulinzi zalia wateja wamekataa kulipia huduma

April 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

Kampuni za walinzi wa nyumbani almaarufu ‘masoja’ zimeathirika kimapato wakati huu wa janga la virusi vya corona.

Kwa mujibu wa kampuni ya Jemal Security, ambayo inahudumia wakazi katika maeneo kadhaa katika kaunti ya Nairobi, wateja “wanachelewa kulipa ada ya usalama na wengine wameamua kutolipa kabisa ada hiyo.”

Mlinzi kutoka kampuni hiyo Ngome Mbangah, ambaye anasimamia mtaa wa Kariobangi South Civil Servants, anasema wateja wanasema mishahara yao imechelewa. Wengine, Mbangah anasema, wanasema wameamua kuchukua hatua hizo kwa sababu biashara zao hawaletei faida.

“Kuna wengine wanasema walipoteza kazi punde tu serikali ilipotangaza kuweka kafyu ya kutoka saa moja usiku hadi saa kumi na moja asubuhi,” Mbangah anasema.

Pia, kuna kundi la wateja, ambalo Mbangah anasema linatumia hali ilioko nchini sasa kuwa wasumbufu. “Wateja wengine wanatumia hali tuliomo sasa kama sababu ya kukwepa ulipaji wa ada ya usalama.”

Hali hii, afisa huyo aliambia Taifa Leo, inaathiri shughuli za kampuni hizo kutoa huduma inayofaa kwa wafanyikazi wao na hata pia wateja “wakati fedha zinazohitajika hazipatikani kwa wakati ufaao”.

“Tunaweka usalama maeneo tofauti katika kaunti ya Nairobi yakiwemo katikati mwa jiji na mitaa ya Umoja, Kariobangi, City Cabanas na Embakasi.

“Ada ya usalama hutegemea na usalama wa eneo husika; kuna maeneo hatari na yale ambayo hatari ni ndogo,” anasema afisa huyo.

Kuchelewa kulipwa ada hii, anasema, husababisha motisha ya wafanyikazi kurudi chini kwa kuwa mishahara yao hucheleweshwa.

“Pia, inaweza kufanya mteja asipokee huduma inayofaa kwa sababu utendakazi pia huathiriwa na maslahi ya wafanyakazi wetu. Hali hii inakumba kampuni zote kwenye sekta hii, haswa kampuni ndogo ambazo bado hazijaimarisha miundomsingi za operesheni ya usalama,” anasema.

“Wakati pesa zinapochelewa kulipwa, inabidi sis kama kampuni kutumia njia mbadala ya kuwalipa wafanyikazi, huku tukingoja wateja kulipa madeni ambacho sio kitu rahisi.”