• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Corona ilivyozima ndoto za vijana

Corona ilivyozima ndoto za vijana

Na Steve Mokaya

Huku gonjwa la COVID-19 likizidi kusagaa ulimwenguni kote na kuwaathiri walimwengu mbalimbali, vijana humu nchini wamehisi kwa kishindo kikubwa athari zake kadhalika.

Wengi wa vijana wanaolia kuhangaisha na hali ya sasa ni wanafunzi wa vyuo vikuu, ambao sasa, kama wanafunzi wote nchini, wako nyumbani.

Kutokana na kuenea kwa virusi vya corona, serikali imeweka mikakati mbalimbali ili kukabili usambazaji wa virusi hivi.

Mikakati hiyo, ambayo ni pamoja na kutokuwa kwenye vikundi vya watu wengi, kusalia majumbani na kadhalika, imewaathiri wengi wa vijana, na wanapoeleza, wanapitia kipindi kigumu.

Baadhi yao walizungumza na Taifa Leo Dijitali kwa njia ya simu. Dianah Nyaboke (pichani) ni binti kifungua mimba katika familia yao. Kabla ya gonjwa la COVID-19, alikuwa katika harakati za kutafuta ajira ili angaa akidhi mahitaji yake.

Chamko la virusi vya corona humu nchini lilisambaratisha mikakati hiyo, na sasa imembidi asalie nyumbani kwao, katika gatuzi la Nyamira, na familia yake.

Ila mambo hayajakuwa rahisi kwake. “Huku nyumbami hamna pesa hata kidogo. Ile kidogo niliyokuwa nayo nilishatumia ikaisha na ikiisha zingine haziingii,” anasema.

“Kadhalika, hata kuongea na marafiki kumekuwa kugumu maana hata pesa ya kununua mjazo wa simu ni shida na huwezi ukaomba kila siku. Mtakosana na mzazi,” anaongeza.

Mbali na uhaba wa pesa za matumizi, Nyaboke anasema kuwa kulazimishwa na hali kukaa nyumbani kumepelekea mzozano na ndugu zake wadogo, kwa mambo madogo madogo kama vile kupigania kiangazambali na kubishana kuhusu nani atakayefanya kazi fulani na fulani za nyumbani, mathalan kuleta maji kutoka mtoni.

Ila, anasema kuwa kwa sasa anajishughulisha kusoma vitabu ili kubisha muda na pia kujaza benki lake la elimu.

Tony Kirimi ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo kikuu ambaye pia analalamikia hali ilivyo. Kwa sasa, Tony yuko nyumbani kwao, katika kaunti ya Meru, na kama wengine wengi, analilia uhaba wa senti za kutumia, kwa angaa kujaza simu.

Isitoshe, anasema ni vigumu kwake kuingia mtandaoni kwa sababu kuna uhaba wa pesa za kununua data bundles na hamna wi-fi kama ilivyo chuoni.

“Hata kukaa nyumbani ni shida maana hakuna marafiki na kuna uchovu usio na mwisho. Halafu, huku nyumbani ni kama siku zote zafanana; hata wikendi ikifika huenda usijue,” anasema.

Fauka ya hayo, anasema kuwa imekuwa vigumu kwake kufanya ibada nyumbani.

“Nilikuwa nimezoa kuhudhuria kanisa lenye waumini wengi huko chuoni ila sasa mambo ni tofauti kwa sababu imebidi tuwe tukifanya ibada ya familia pekee, na kuzoea si rahisi,” anaongeza.

Licha ya kuwa shule zote zimefungwa, Tony anasema kuwa baadhi ya wahadhiri katika chuo chao wanazidi kuwatumia kazi za kufanya, na muda wa kuzifanya ni mchache mno.

Isitoshe, wanafunzi wenzake hawajafurahishwa na hatua hiyo, licha ya kuwa wanatamani shule zifunguliwe haraka iwezekanavyo.

“Wanafunzi wengi wanalalamikia kazi hizo kwa sababu wengi wao hawawezi kuingia mtandaoni, na kazi zenyewe zinatumwa kwa mtandao huo huo. Kadhalika, hata inakuwa vigumu kufanya utafiti wa kazi zinazotumwa,” anasema.

Halikadhalika, Catherine Muyonga kutoka mjini Mumias, ambaye pia ni mwanafunzi wa chuo kikuu analalamikia kipindi hiki kwa vile kimesambaratisha mipango aliyokuwa nayo ya kujiendeleza kimasomo na hata kikazi.

Anasema kuwa mbali na kazi za nyumbani, hamna jambo lingine analojishughulisha nalo.

“Huwa napenda kusoma vitabu, na hasa riwaya, ila sasa ni kama nimemaliza kusoma vyote nilivyoikuwa navyo,” anasema.

“Halafu pia napenda kuoka keki ila sasa sina pesa za kutosha za kununua vifaa na hasa viungo. Isitoshe, nyumba imejaa kila wakati na ni vigumu kupata muda wako binafsi. Zaidi ya hayo, nguvu za mawimbi ya mtandao ni dhaifu mno na inakuwa vigumu kuingia katika mitandao ya kijamii. Maisha magumu kweli,” anaongeza.

Fauka ya hayo, anasema kuwa hali hii imeathiri uhusiano na mpenziwe kwa muda sasa; maana hawawezi kupatana, na kuwa maongezi ya kila siku ya simu yanaelekea kuchosha na kuwa kama kawaida.

Erick Ongaki, mwanafunzi wa somo la maabara katika chuo kikuu cha MKU, ambaye sasa anafanya kilimo katika eneo la Mwea, anasikitikia hali hii kwa vile imepunguza kasi ya uzalishaji wa vyakula vyake shambani.

“Imeniwia vigumu kununua vifaa vya shambani kutoka Nairobi. Aidha, bei ya vyakula kama mboga hapa imepanda maradufu na hakuna pesa za kutosha. Zaidi ya hayo, agizo la kuzingatia umbali wa mita moja baina ya limeathiri mradi wangu wa shambani sana kwa sababu siwezi kuajiri watu wa kutosha ili wanisaidie. Bila shaka hilo limeathiri mazao yangu,” anasema.

Kutokana na agizo la serikali kuwa watu wasalie majumbani, Ongaki anasema kuwa kazi yake ya kujitolea ya kuwatembelea na kuhubiria majirani kutoka kwa nyumba moja hadi nyingine imepigwa breki huko Mwea aliko.

Kwa upande wake, Kezia Onsongo, mkazi wa Nyamira, anasema kuwa COVID-19 imesambaratisha mpango aliokuwa nao wa kufungua biashara ya kuuza mavazi.

Kezia, ambaye ni mama wa mtoto mmoja, anasema hata shughuli ya malezi humwia ngumu, bila pesa za kutosha.

“Kwa vile sina kazi, nategemea watu wanitumie pesa, na wakati mwingi hizo pesa haziingii haraka zinavyohitajika. Wakati mwingine mtoto huwa mgonjwa na naogopa kumpeleka hospitali, kwa vile naweza kumpeleka na apatwe na virusi vya corona kuko huko hospitalini.

“Zaidi ya yote, hali hii imeniletea upweke kwa vile wazazi wangu hawawezi kututembelea wala sisi hatuwezi kuenda huko waliko katika eneo la Magharibi,” anasema

Yote tisa, kumi ni kuwa athari za ugonjwa huu na hali inayoambatana nao zimemfikia kila mja, na hakuna dalili za hali ya kawaida kurejelea hivi karibuni.

Hata hivyo, huu si mwisho wa maisha. Basi ni jukumu la kila mtu, na hasa vijana kuikumbatia hali ili angaa kupunguza makali yake. Huku tukifanya hivyo, sote twafaa tuishi na tumaini kuwa ipo siku mambo yatakuwa sawa.

Hiyo siku itakuwa siku njema, chambilecho marehemu Prof Ken Walibora.

You can share this post!

Abiria wataka huduma za treni Nairobi ziendelee kama kawaida

Serikali yaonya wakazi wa Kiambu, Murangá, Machakos na...

adminleo