Michezo

Chelsea yahemea huduma za Aubameyang wa Arsenal

April 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Frank Lampard amefichua kwamba kikosi chake cha Chelsea kitakuwa sokoni mwishoni mwa msimu huu kujinasia huduma za fowadi Moussa Dembele wa Olympique Lyon nchini Ufaransa au Timo Werner wa RB Leipzig, Ujerumani.

Ingawa hivyo, Chelsea huenda wakazihemea huduma za Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal iwapo wataambulia patupu katika juhudi za kupigania maarifa ya wavamizi hao wawili ambao ni vivutio kwa Lampard.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Aubameyang alidokeza uwezekano wa kuagana na Arsenal iwapo kikosi hicho kitashindwa kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao. Na ilivyo, hivyo ndivyo hali itakuwa.

Japo Arsenal wanatazamiwa kuanzisha mazungumzo na Aubameyang kwa nia ya kumsadikisha arefushe mkataba wake ugani Emirates, dalili zote zinaashiria kwamba nyota huyo wa zamani wa Borussia Dortmunda atapania kutafuta hifadhi kwingineko.

Hii ni baada ya Rais wa Shirikisho la Soka la Gabon, Pierre Alain Mounguengui, kumtaka nahodha huyo wa Arsenal, na timu ya taifa ya Gabon kujiunga na kikosi cha haiba kubwa zaidi kitakachomwezesha kufikia mengi ya matamanio yake kitaaluma.

Baada ya kushuhudia aliyekuwa mchezaji wao wa haiba kubwa, Aaron Ramsey, akijiunga na Juventus bila ada yoyote msimu jana, Arsenal wasingetaka kurudia kosa la kumdumisha zaidi sogora yeyote aliye na mkataba wa chini ya miezi 12 kikosini mwao.

Mkataba wa sasa kati ya Arsenal na Aubameyang, 30, unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Aubameyang alipokezwa ukapteni wa Arsenal mnamo Novemba 2019 baada ya kiungo Granit Xhaka kupokonywa utepe huo kwa sababu ya utovu wa nidhamu.

Ingawa kocha Mikel Arteta amewataka Arsenal kutomtia Aubameyang mnadani, huenda waajiri wake wa sasa wakalazimika kufanya hivyo ili kujipatia fedha zitakazowawezesha kujisuka upya kwa minajili ya misimu ijayo.

Iwapo itawawia vigumu kuwauzia wapinzani wao wakuu mvamizi huyo, basi Arsenal watakuwa radhi kufanya biashara na Inter Milan au Barcelona ambao wamefichua azma ya kumtia Aubameyang katika sajili rasmi ya kikosi chao iwapo watayakosa maarifa ya Lautaro Martinez wa Inter Milan.

Huku Inter Milan ya kocha Antonio Conte ikimtaka Aubameyang awe kizibo cha Martinez anayemezewa na Barcelona, Barcelona pia wanamsaka mrithi cha kigogo wa timu ya taifa ya Uruguay, Luis Suarez.

Hilo litakuwa pigo kubwa kwa Chelsea ambao wanaona bei ya Aubameyang kuwa nafuu zaidi kuliko ya Dembele au Werner anayeviziwa pia na Liverpool.

Huku ada ya kumsajili Dembele na Werner ikiwa takriban Sh11 bilioni, Arsenal wapo radhi kuzinadi huduma za Aubameyang kwa Sh5.6 bilioni pekee kutokana na umri wake unaozidi wa Dembele na Werner kwa miaka saba zaidi.

Licha ya umri huo, Aubameyang amekuwa mwepesi wa kutikisa nyavu za wapinzani wao nchini Uingereza, huku akijivunia kwa sasa mabao 17, mawili pekee nyuma ya Jamie Vardy wa Leicester City anayeongoza orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Aubameyang alipachika wavuni jumla ya mabao 22 katika EPL msimu uliopita na kutawazwa mfungaji bora wa kivumbi hicho kwa pamoja na Sadio Mane na Mohamed Salah wa Liverpool. Mane na Salah pia ni wachezaji wa timu za taifa za Senegal na Misri mtawalia.

Kwa sasa, Aubameyang hupokezwa mshahara wa hadi Sh28 milioni kwa wiki uwanjani Emirates huku Dembele akitia mfukoni nusu ya fedha hizo kila baada ya siku saba nchini Ufaransa.

Ingawa Chelsea walikuwa awali wakihusishwa na chipukizi Jadon Sancho, dalili zinaashiria kwamba chipukizi huyo wa Dortmund yuko radhi tayari kutua Manchester United kuliko Chelsea ambao tayari wametishwa na bei yake ya Sh17 bilioni.

Olivier Giroud anatarajiwa kuagana na Chelsea bila ada yoyote mwishoni mwa msimu huu baada ya ushirikiano wake na Michy Batshuayi kushindwa kuzalisha matunda ya kuridhisha. Kubanduka kwake kunamsaza chipukizi Tammy Abraham, 22, kuwa mshambuliaji pekee wa kutegemewa zaidi kambini mwa Chelsea.

Hadi kusitishwa kwa kipute cha EPL msimu huu kutokana na mlipuko wa virusi vya corona, Aubameyang alikuwa amewafungia Arsenal jumla ya magoli 20 katika mashindano yote ya Uingereza na Ulaya.

Tangu ajiunge na Arsenal kwa kima cha Sh7.8 bilioni kutoka Borussia Dortmund mnamo Januari 2018, Aubameyang ameshuhudia kikosi chake kikibanduliwa kwenye fainali za Europa League na Carabao Cup; na bado hajanyanyua taji lolote ugani Emirates.