• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
TAHARIRI: Heko Rais Uhuru kwa kuwajali pia wanaspoti wetu

TAHARIRI: Heko Rais Uhuru kwa kuwajali pia wanaspoti wetu

Na MHARIRI

MNAMO Jumatano, Rais Uhuru Kenyatta hatimaye aliyasikia malilio ya wengi kuhusu wanamichezo wa Kenya waliopata pigo kubwa kimapato kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona almaarufu Covid-19.

Rais aliagiza Hazina ya Michezo (Sports Fund) itumike kupata pesa zitakazotumiwa kuwaruzuku wanamichezo wetu ambao wamepoteza riziki kutokana na janga hili.

Hatua hiyo ilifuatia vilio vya wengi walioshangaa sababu ya Rais Uhuru kuwajali wasanii pekee alipoamuru wapewe Sh100 milioni kila mwezi huku sekta ya michezo ambayo pia ina vijana wengi ikisahaulika kabisa.

Naam, haikuwa makosa kwa Rais Uhuru kuwapokeza wasanii pesa kwa dhamira ya kuwatumbuiza wananchi wakati huu wa tishio la corona, lakini busara ingemwelekeza kuwakumbuka pia wanamichezo ambao sasa hawawezi kumudu maisha baada ya shughuli zote za michezo kusimamishwa nchini na kwingineko duniani.

Hali hiyo iliwatupa vijana katika lindi la masumbuko wasijue ni wapi pa kukimbilia ili kujiokoa na makali ya njaa pamoja na majakamoyo yanayotokana na ukosefu wa pesa.

Iwapo Rais angechelewa kuchukua hatua hiyo, kulikuwa na dalili maridhawa kwamba baadhi ya vijana walioathiriwa wangeamua kuingilia vitendo vya uhalifu ili kujiokoa na balaa hili.

Baada ya tangazo hili, sasa kinachosubiriwa ni, lini wanamichezo hao watakapoanza kupata hela yao.

Kuchelewa kuwafikisha fedha hizo pia kunaweza kuwa chanzo cha maafa mengi pamoja na uhalifu.

Hata kama ni kidogo, sharti serikali iharakishe kuwagawa vijana pesa hizo ili waanze kuyakwamua maisha yao -chelewa chelewa utamkuta mwana si wako.

Naam twajua kwamba huenda pesa hizo zisiwafikie wahusika wengi jinsi inavyoweza kufaa. Hivyo basi ni muhimu kutumia hazina nyinginezo kuwafikia vijana wengine ambao maisha yao yametatizika kutokana na maradhi haya.

Maadamu mfuko wa spoti pekee huenda usiwatoshe wanamichezo wote, ni muhimu serikali iangalie hazina nyinginezo kama vile Mfuko wa Vijana na Kinamama katika juhudi za kuauni makundi mengineyo ya vijana ambayo hayatafikiwa na hela za Hazina ya Spoti.

Japo taifa hili letu linapitia changamoto kubwa ya kiuchumi hasa kutokana na zigo kubwa la madeni, twasadiki kuwa bado zipo njia ambazo serikali inaweza kutumia kuwaokoa vijana wengi dhidi ya upungufu mkubwa wa pesa unaowaathiri Wakenya kwa sasa.

Serikali inaweza kufuata ushauri wa wataalamu kuhusu mbinu mbalimbali zinazoweza kutumika kwa sasa kuwaokoa raia wengi waliopoteza riziki kutokana na janga hili.

Mmoja wa wataalamu hao ni mwanauchumi mahiri Dkt David Ndii aliyependekeza njia mbalimbali zinazoweza kutumiwa na serikali kusaidia raia walionaswa katika utando huu wa corona.

Mojawapo ya njia hizo ni kuruhusu benki ziyakopeshe mashirika yote yaliyoathirika na ugonjwa huu kiasi cha pesa ambacho kinaweza kutumiwa kulipa mishahara na marupurupu ya wafanyakazi.

Anavyoeleza, mkopo wa aina hiyo usiwe na masharti yoyote magumu wala riba na uanze kulipwa baada ya janga hili kutokomezwa.

Inapozingatiwa kuwa benki hupata pesa za kukopesha raia kutoka kwa Benki Kuu ya Kenya (CBK), inabainika kuwa pesa zilizo katika benki hiyo kuu ni za umma, kwa hivyo katika hali kama hii, ni bora wananchi wapewe ili mambo yatakapotengenea, warudishe bila masharti, tena wapewe kipindi kirefu cha kulipa mikopo hiyo.

Miongoni mwa mashirika yaliyoathirika zaidi ni klabu za michezo ambazo kwa hakika zitasaidiwa pakubwa kwa kukopeshwa pesa zisizokuwa na masharti halafu zirejeshwe baadaye.

Yote yawezekana.

You can share this post!

ASHUKA BEI SH4B: Coronavirus yashusha bei ya Pogba kwa Sh4...

Chelsea yahemea huduma za Aubameyang wa Arsenal

adminleo