• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
COVID-19: Wahudumu wa bodaboda Githurai 45 walia ‘maisha magumu’

COVID-19: Wahudumu wa bodaboda Githurai 45 walia ‘maisha magumu’

Na LAWRENCE ONGARO

WANABODABODA wa Githurai 45 wana sababu ya kulalamika wakidai hali ya maisha imekuwa ngumu.

Wanasema kuwa kwa muda wa mwezi mmoja sasa biashara yao imezorota ajabu maisha yakigeuka kuwa kitendawili.

Wanazidi kueleza ya kwamba pesa za kujikimu kimaisha zinakosekana.

Mhudumu wa bodaboda katika eneo hilo, Bw Samuel Ngugi anasema hapo awali alikuwa akipata Sh1,500 kwa siku, lakini anasema kwa sasa anaweka mfukoni Sh200 pekee.

“Ninaporudi nyumbani jioni ninashindwa kueleza mke wangu jinsi mambo yalivyo. Kwa hivyo, tumebaki na upweke,” akasema Bw Ngugi.

Naye Bw Amos Gachara anasema hata hawaelewi – wahudumu hao – jinsi watakavyolipa mikopo yao.

“Muda wa kazi umebadilika sana ambapo tunalazimika kufanya saa chache tukilinganisha na hapo awali,” akafafanua Bw Gachara.

Ombi lao kuu kwa sasa ni serikali pia iingilie kati ili kuokoa wanabodaboda ndiposa waweze kupata afueni.

Anasema viongozi wajitokeze ili kuwapiga jeki kwa sababu familia zao ziko katika hali ngumu ya maisha.

Bw Gachara anatoa changa moto kwa viongozi hasa wa kisiasa wajitokeze wazi kwa kuwasaidia wanabodaboda ambao kwa sasa wako katika hali ngumu kimaisha.

“Wakati wa siasa wao huwa mstari wa mbele kununulia vijana T-shirts, na kofia za kampeni, kwa hivyo huu pia ndiyo wakati wao wa kuonyesha ukarimu wao kwa vijana mashinani,” alifafanua Bw Gachara.

Alisema hii kafyu imebadilisha hali yao ya maisha ambapo pesa hazionekani mifukoni inavyostahili.

“Tunaporejea nyumbani jioni tunahisi uzito kukidhi mahitaji kwa sababu pesa kidogo tunazopokea kutoka kwa kibarua hata hazitoshi kununua chakula cha familia,” alijitetea mwanabodaboda huyo.

Alisema hata kuna watu wengine wamelazimika kusitisha kazi hiyo kwa sababu barabara nyingi hazipitiki kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha usiku na mchana.

You can share this post!

Ligi Kuu Uholanzi yafutwa, hakuna mshindi

Rais avunja itifaki

adminleo