Michezo

Kenya kupoteza mabilioni kutoka kwa wanariadha kwa sababu ya corona

April 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

WANARIADHA wa Kenya watapoteza zaidi ya Sh5 bilioni wanayopata mashindanoni kama tuzo za washindi, matangazo ya kibiashara ama haki za picha zao kutumiwa, marupurupu ya muda bora na ada ya kujitokeza.

Huo ni utathmini wa Mwenyekiti wa tawi la Nairobi la Shirikisho la Riadha Kenya, Barnaba Korir.

Gazeti la The Strait Times limemnukuu Korir akisema, “Mbali na fedha wanazopata katika kandarasi zao za kila mwaka, wanariadha watapoteza tuzo, ada ya kushiriki mashindano na matangazo kutoka kwa kampuni zinazotaka kuwatumia kutangaza bidhaa zao. Ni pigo kubwa kwa uchumi wa Kenya.”

Hawa hapa ni baadhi ya wanariadha waliovuna vinono mwaka 2019:

Lawrence Cherono alijishindia Sh16 milioni na Sh10.6 milioni kwa kunyakua mataji ya mbio za kifahari za Boston na Chicago nchini Marekani, mtawalia.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 Eliud Kipchoge alihifadhi ubingwa wake wa London Marathon nchini Uingereza kwa rekodi mpya ya London Marathon ya saa 2:02:39 akijizolea Sh5.8 milioni tuzo ya mshindi na Sh10.6 milioni kwa kukamilisha umbali huo chini ya saa 2:05:00. Ingawa kitita alichotunukiwa kuwa mtu wa kwanza kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili alipotimka 1:59:40 mjini Vienna nchini Austria kinasalia siri, Kipchoge anaaminika alikula vizuri sana katika mbio hizo maalum.

Nao Geoffrey Kamworor na Joyciline Jepkorir walibeba mataji ya New York Marathon nchini Marekani na kuzawadiwa Sh10.6 milioni kila mmoja.

Brigid Kosgei alivuna Sh18.7 milioni kwa kutwaa taji la Chicago Marathon kwa rekodi mpya ya dunia ya mbio za kilomita 42 za wanawake ya saa 2:14:04 na Sh13.8 milioni kwa kushinda London Marathon chini ya saa 2:20:00 (2:18:20).

Ruth Chepngetich alivuna Sh9.6 milioni kwa kushinda Vodafone Istanbul Marathon nchini Uturuki na Sh6.4 milioni kwa kuibuka malkia mpya wa Riadha za Dunia jijini Doha nchini Qatar.

Hawa ni baadhi tu ya wakimbiaji kutoka Kenya walionyakua mataji mwaka 2019. Kenya ina zaidi ya watimkaji 1,000 wanaoshiriki mashindano kote duniani. Kwa sasa, mashindano mengi yamesimamishwa kwa sababu ya virusi vya corona. Baadhi ya mashindano yamefutiliwa mbali, ingawa mengi yameahirishwa kwa tarehe mpya, ambazo pia huwezi kujua kama janga hili litakuwa limeisha ama sababu zisizoweza kuepukika kuwaweka nje.