Maaskofu wa kanisa Katoliki waitaka serikali itenge fedha iwafae waathiriwa wa mafuriko
Na CHARLES WASONGA
MAASKOFU wa Kanisa Katoliki wameitaka serikali kutenga rasilimali za kutosha kuwafidia Wakenya walioathirika na mafuriko katika kaunti za Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet, Kisumu, Siaya na Bungoma.
Tume ya Haki na Amani ya Muungano ya Maaskofu wa Kanisa hilo (KCCB) pia imetoa wito kwa Wakenya wenye uwezo wawasaidie wananchi walioachwa bila makao hasa wakati huu ambapo taifa linapambana na janga la virusi vya corona.
Jumla ya watu 28 wameripotiwa kufariki katika mafuriko na maporomoko ya ardhi katika eneo la Chesogon lililoko mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo kuanzia Alhamisi wiki jana.
“Tunazitaka ngazi zote za serikali kutenga fedha kwa dharura za kuwasaidia waathiriwa wa mikasa hii,” ikasema taarifa ya tume hiyo iliyotiwa saini na mwenyekiti wake Kasisi John Oballa Owaa.
Hata hivyo, tume hiyo ya Haki na Amani ilitoa wito kwa wananchi kwenye maeneo yenye hatari ya kuathiriwa na mafuriko, kuzingatia ilani iliyotolewa na Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga ili kuzuia maafa ya uharibifu wa mali.
“Usalama huanza na mtu binafsi pamoja na jamii kabla ya serikali kuingilia kati,” akaeleza Kasisi Owaa.
Zaidi ya familia 400 zimeachwa bila makao katika kaunti zilizoathiriwa na mafuriko huku baadhi yao wakiendelea kuwasaka wapendwa wao ambao bado haijulikani waliko.
Picha za madhara yaliyosababishwa na mafuriko zimekuwa zikipeperushwa katika runinga za humu nchini baada ya mito kuvunja kingo zao maeneo mbalimbali nchini.
Wiki jana Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini ilionya kuwa mvua kubwa itaendelea kushuhudiwa katika maeneo ya Magharibi mwa nchi, Kati, Pwani na Nairobi kwa siku kadha zijazo.
Imewataka watu wanaoishi katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko na maporomo ya ardhi kuhamia sehemu salama.