Makala

SUSAN NJOROGE: Sipendi raha za dunia

April 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

NI miongoni mwa wasanii wanaoibukia katika ulingo wa burudani ya nyimbo za kumtukuza Mungu. Talanta yake ilitambuliwa akisoma darasa la nne kwenye Shule ya Michore, Ol Kalou Nyandarua.

Hata hivyo, Susan Nyakio Njoroge maarufu kama Suzzy anasema analenga kufikia upeo wa wanamuziki mahiri Afrika Afrika kama Christina Shusho kati ya wengine.

”Ninahisi ninacho kipaji tosha katika utunzi wa nyimbo za injili,” amesema na kuongeza kuwa katika utunzi wake hutegemea Mungu kumpa ufunuo wa fataki zake.

Aidha anasema analenga kuendelea kutunga nyimbo zinazosheheni maudhui ya kujenga Wakristo kiroho. Suzzy alimpokea Kristo kuwa mwokozi wa maisha yake mwaka 2018.

”Binafsi nililelewa katika maisha ya Kikristo wala sijawahi vutiwa na maisha ya raha za hapa duniani hali iliyonipa msukumo tosha kumkaribisha Kristo kuwa kiongozi wa maisha yangu,” alisema na kuongeza kuwa ndani ya wokovu wake anajivunia mengi ikiwamo ufunuo wa teke zake maana huwa sio maneno yake binafsi.

Anasema nyimbo zake huja anaposoma Biblia pia kama ndoto. Pia anasema kila anapomwomba Mungu umtimizia mahitaji yake.

ALBAMU MOJA

Msanii huyu aliyezaliwa mwaka 1990 anasema tangia akiwa mtoto alitamani kuhitimu kuwa mkuu wa mojawapo ya taasisi za masuala ya elimu lakini maisha yalimwendelea mramba. Mbali na uimbaji msichana huyu amehitimu kwa shahada ya diploma katika usanifu wa picha na maumbo pia masuala ya kompyuta.

Kisura huyu mwenye umbo la kuvutia amerekodi na kutoa albamu moja yenye kichwa Riria Ndetikirire (Wakati nilimpokea Kristo) inayojumuisha fataki sita.

Orodha yazo ikiwa: ‘Riria Ndetikirire (Wakati nilimpokea Kristo),’ ‘Maundu (Mambo),’ ‘Ndiinaga na Gikeno(Nitakuwa naimba kwa furaha),’ ‘Uthamaki (Ufalme),’ ‘Mutharaba (Msalaba),’ na ‘Ona ndona Thina (Hata nikipata shida).’

Msanii huyu anasema kwa wasanii wa humu nchini huvutiwa nao Sarah K na Ruth Wamuyu watunzi wa ‘Mnyunyizi wangu,’ ‘Usiyeshindwa,’ na ‘Amukira ngatho,’ ‘Wi muthaka,’ mtawalia.

Katika Ukanda wa Afrika Mashariki anapenda sana kusikiza fataki za wanamuziki kama Christina Shusho na Rose Muhando waghani wa teke kama ‘Ninang’ara,’ ‘Wakuabudiwa,’ na ‘Utamu wa Yesu,’ ‘Mpe Bwana Utukufu,’ mtawalia.

CHANGAMOTO

Anasema hupitia pandashuka nyingi tu kwenye juhudi za utunzi wao ikiwamo kukosa fedha za kugharamia ada ya kurekodi nyimbo zao. Pia kwa wale hawana mwito hujipata kwenye wakati mgumu maana kutunga nyimbo sio rahisi.

”Ninaamini kuwa na mwito husaidia pakubwa hasa kupata ufunuo katika masuala ya utunzi,” anasema na kuongeza kuwa baadhi ya wafuasi wao wanapenda kuwaponda kulingana na fataki zao.

USHAURI

Anashauri wasanii wa injili wanaokuja kuwa makini katika kazi zao maana wanapaswa kughani nyimbo za kujenga Wakristo kiroho.

Pia anasema muziki wa injili unayo nafasi ya kupiga hatua hapa Kenya anakosema Serikali inastahili kuweka mikakati mwafaka kuzima wauzaji wa muziki ghushi.

Anasema huwa inasikitisha sana msanii kurekodi nyimbo yake na kabla ya kuiachia kuipata madukani ikiuzwa. Binti huyu aliyesomea Shule ya Upili ya Ndemi anasema yungali singo ambapo kwa yote anatarajia Mungu ampe Mume ameokoka.