• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
AKILIMALI: Ukuzaji miche unalipa

AKILIMALI: Ukuzaji miche unalipa

Na JOHN NJOROGE

[email protected]

Unapoingia mji wa Elburgon kupitia barabara mbovu ya Molo- Nakuru unapata aina tofauti ya miti kwa upande wa kushoto ambayo imeizungaka sehemu ndogo iliyopandwa miche ya aina mbalimbali.

Katika sehemu hiyo ya shamba, tunampata mwenyewe, Daniel Ndung’u akiwa kazini.

Huku amevalia shati ya malai, koti ya kahawia,viatu vyeusi na suruali ndefu, Ndung’u alikuwa katika harakati ya kushughulikia miche aliyoipanda katika sehemu ya mita 50 kwa 100.

“Nimepanda miche 42,000 ambayo ni aina tofauti ya miti, maua na matunda baadhi ya nyingine nyingi,’’ akasema bwana Ndung’u anayejishughulisha na miche ya miti kwa wingi.

Daniel Ndung’u aonyesha miche yake iliyoharibiwa baada ya mvua ya mafuriko kunyesha hivi majuzi mjini Elburgon katika kaunti ya Nakuru. Alikapata hasara zaidi ya shiling 380,000. PICHA/JOHN NJOROGE

Alisema kuwa aliipata shauku ya miche mwaka 2008 alipoipanda miche hiyo. Kwa wakati huo, alikuwa anafanya kazi ya kibarua katika msitu wa Mariashoni, ambao kwa hivi sasa hutambulika kama msitu wa Mau.

Akiongea na Akili Mali hivi majuzi, Ndung’u alisema kuwa kazi hiyo ya kibarua haikwenda mbali kabla serikali ya wakati huo ilipoanza kutenga msitu huo ambao jamii mbili za Ogiek na Kipsigis zilianza kutulia kwenye msitu huo.

“Niliacha kazi ya kibarua na kutulia kwenye kitalu changu. Wizara ya Kilimo ilikuwa imetekeleza asilimia kumi ya msitu kwa yeyote ambaye angelima na kupanda miti katika mashamba ama msitu huo,’’ akasema.

Aliongeza kuwa aliona ni wakati mzuri wa kuwauzia waliokuja kutulia kwenye msitu huo miche yake ya miti ambayo alikuwa ameipanda kwa wingi na iliyokuwa inahitajiwa kwa hali na mali na watu wengi.

Kwa muda wa mwezi mmoja uliopita tangu kuzuka kwa virusi vya Korona ambavyo vimesababisha vifoo vya watu wengi ulimwenguni, bwana Ndung’u amesema kuwa zaidi ya miche 10,000 imekua kupita kiasi ambayo ingempa zaidi ya shilingi elfu mia moja (100,000) kutoka kwa mauzo yake.

“Baadhi ya wateja wangu walitoka nje ya kaunti ya Nakuru. Nilikuwa na wengine ambao walisafiri kutoka kaunti ya Nairobi kuja kununua miche. Sehemu hiyo ni moja ya zile zimepigwa marafuku kutoka nje ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Korona,’’ akasema bwana Ndung’u.

Kutokana na marufuku hayo, wengi wa wateja wake hawapati nafasi ya kumtembelea kwenye sehemu yake ya miche. Aliongeza kuwa hata wale majirani wake waliomtembelea kuja kununua miche hawana chanzo cha kupata pesa kutokana na janga hilo la Korona.

“Biashara nyingi zimefungwa kwa minajili ya kuzuka kwa virusi vya Korona. Baadhi ya biashara hizo zilizofunguliwa hata masaa ya usiku kama vile mikahawa na vilabu zimefungwa kufuatia maagizo ya serikali,’’ akasema.

Alikiri kuwa wateja wake wa karibu waliofanya kazi za vibarua wamepungua pia. Alisema kuwa pesa chache ambazo waakazi hao wanazipata hazitoshi hata kukidhi familia zao.

Mkulima huyu alitarajia kupata zaidi ya sSh380,000 za mazao ya miche ifikapo mwezi wa nane mwaka huu. Alisema kuwa mauzo mengi huonekana kati ya mwezi wa Machi na Aprili kila mwaka wakati wa msimu wa kupanda.

Kila miche huuzwa kwa bei tofauti kulingana na aina ya miche ya miti na matunda.

Miche ya kigeni huuza kati ya shilingi kumi na ishirini ilihali kwa ile ya asili huuza kati ya shilingi thelathini na hamsini. Miche ya matunda na maua, huuza kwa bei tofauti pia.

Naye bwana Nelson Gatheru ambaye pia ni mtaalam wa miche alisema kuwa tangu ujio wa serikali ya ugatuzi, wakulima walikuwa wanapewa mafunzo ya bure kutoka kwa maafisa wa misitu za wilaya katika enzi hizo ambapo walitembea sehemu nyinginezo na kupata mafunzo na ujuzi mwingi wa kupanda na kukuza miche.

“Tulikuwa tunapewa miche bila malipo, vyombo vya kunyunyizia maji, toroli baadhi ya vyombo vingine vya kutayarisha kitalu. Kwa wakati huo, hakuna mkulima aliyeshuhudia miche yake kukua kupita kiasi kama tunavyoona kwa sasa,’’ akasema Bw Gatheru.

Alisema kuwa miche ya kigeni ni chache kwenye kitalu hiyo ikilinganishwa na miche ya asili ambayo ina wateja wengi. Wakulima wengi hununua miche ya kiasili ambayo baada ya kukomaa, huuza ama hupata mauzo kwa haraka.

Gatheru aliongeza kuwa kila mwaka, serikali kuu hutoa fedha za kuhifadhi mazingira lakini tangu mwaka wa 2017 pesa hizo hazijawafikia.

“Fedha hizo huwasaidia wana biashara wa miche ambao familia zao zinawategemea. Tungeomba serikali ya kaunti ifufue fedha hizo na kufungua soko ambayo ndio changa moto kubwa kwa wakulima wa miche ili wapate kujimudu kimaisha,’’ akasema Gatheru.

Kwa upande wake, bwana Ndung’u alisema kuwa karatasi za nailoni wanazotumia kufunga miche zimekuwa changamoto pia kwa wana miche tangu serikali ilipoipiga marufuku.

Alisema wao hubidi kuyatengeneza upya makaratasi yaliyoko kwa miche iliyokua kupita kiasi na kuyatumia tena kwa kupakia miche.

Maono ya bwana Ndung’u ambaye hutegemea biashara hii katika maisha yake ni kupata shamba lingine kubwa ambalo atalipanda miche ya miti, maua, mboga na matunda kwa wingi na kuitenga sehemu anayoitumia kwa sasa kama mahali pa kuuzia.

Hivi majuzi, bwana Ndung’u alikadiria hasara zaidi baada ya miche yake kubebwa na maji ya mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha katika sehemu hiyo.

Ameiomba serikali ya kaunti kumpa msaada ili aweze kuendelea na ukulima wake wa miche.

Sehemu za Elburgon na Molo wananchi hutegemea kilimo ambacho ndio uti wa mgongo wa nchi hii.

Vijana nao ambao walitegemea kazi ya upasuaji wa mbao wamekuwa wakitaabika na kushughulika kwa hali na mali tangu misitu ilipofungwa na serikali.

Ifikapo msimu wa kupanda, vijana hao hufanya kazi ya vibarua ili kupata pesa za chakula na za kujimudu kimaisha ingawaje baadhi yao hupotea kwa pombe haramu ambayo ndio chanzo cha wengi wao wanaokaa pembeni wakati wa masaa ya kazi.

You can share this post!

SUSAN NJOROGE: Sipendi raha za dunia

BI TAIFA MACHI 02, 2020

adminleo