Habari

Waasi wa sayansi

April 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na MASHIRIKA

IDADI ya marais na viongozi wanaokiuka ushauri wa wanasayansi na madaktari katika kukabili virusi vya corona inaendelea kuongezeka duniani.

Kiongozi wa majuzi kupendekeza tiba potovu ni Rais Donald Trump wa Amerika ambaye amewataka madaktari watafute mbinu za kuwadunga watu sindano yenye dawa za kuua viini.

Dawa hizo ni kama vile Dettol, Robertson, Carex, Harpic, Clorox na Jik.

“Nimesikia dawa za kuua viini zinamaliza virusi vya corona haraka sana. Tunafaa kutafuta jinsi tunavyoweza kudunga dawa hizo kwenye miili ya watu ili ziweze kuosha virusi,” akasema Rais Trump akihutubia wanahabari.

Ukweli wa kisayansi ni kuwa dawa za kuua viini zinamaliza viini vikiwemo vya corona zinaponyunyiziwa, kupanguza ama kusafisha.

Rais Trump pia alipendekeza uchunguzi kufanywa kuhusu iwapo miale ya jua inaweza kutumika kuua viini hivyo mwilini. Hii ni baada ya madaktari kumwambia kuwa miale ya jua inasaidia kuua virusi vya corona.

Pendekezo potovu la Rais Trump ni sawa na la Gavana Mike Sonko wa Nairobi, ambaye alijumuisha pombe aina ya Hennesey kwenye vifurushi vya misaada kwa wakazi wa mitaa ya mabanda jijini Nairobi.

Akitetea hatua yake, Bw Sonko alitoa madai ya uwongo kuwa utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ulikuwa umeonyesha kunywa pombe kunaua viini vya corona mwilini.

“Kama una viini vya corona kooni, ukinywa Hennesey itaua viini hivyo mara moja,” akadai Bw Sonko.

Hii ni licha ya WHO kusisitiza kuwa pombe haina uwezo wa kuponya corona.

Kampuni inayosambaza pombe ya Hennesey nchini pia ilipuzilia mbali madai ya Bw Sonko.

Chama cha Madaktari cha Amerika kilitoa taarifa muda mfupi baada ya hotuba ya Rais Trump kikiwaonya watu dhidi ya kunywa dawa za kuua viini ama kujidunga.

“Haya ni matamshi hatari. Huenda baadhi ya watu wakayachukua kwa uzito wakidhani ni wazo njema,” akasema Craig Spencer wa Chuo Kikuu cha Matibabu cha Columbia.

Kampuni ya Reckitt Benckiser ambayo inatengeneza dawa za kuua viini, pia ilitoa taarifa ikionya dhidi ya watu kunywa ama kujidunga dawa zake.

Trump amekuwa miongoni mwa viongozi ambao wamekuwa na misimamo isiyo ya kawaida katika kukabiliana na virusi vya corona.

Mapema wiki hii Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, alipiga marufuku unyunyizaji dawa za kuua viini nchini humo akisema hazimalizi virusi vya corona.

Rais Magufuli alisema unyunyizaji dawa za kuua viini unaua wadudu kama vile mbu na kombamwiko, wala sio virusi vya corona.

“Hakuna unyunyizaji dawa unaoweza kuua virusi vya corona. Unyunyizaji uliofanyika Dar es Salaam ni ujinga! Huwezi kuua virusi vya corona ukitumia kemikali ya klorini. Hiyo inaua mbu na kombamwiko pekee,” akasema rais huyo.

Alieleza kuwa hakuna thibitisho la kisayansi kuwa virusi vya corona vinamalizwa kwa kunyunyiziwa dawa.

Hii ni licha ya wanasayansi kupendekeza unyunyizaji dawa kama njia ya kukabili corona.

Kulingana na Rais Magufuli, kama unyunyizaji dawa unaua virusi hivyo, basi mataifa ya ng’ambo hayangekuwa na tatizo la Covid-19.

“Iwapo unyunyizaji dawa unasaidia, basi mataifa ya ng’ambo ambayo yamekuwa yakifanya hivyo usiku na mchana yangekuwa yamemaliza kabisa virusi vya corona nchini mwao,” akaeleza Rais Magufuli.

Kiongozi mwingine ambaye amechukua msimamo kinyume na sayansi na madaktari ni Rais Jair Bolsonaro wa Brazil ambaye ametaja Covid-19 kama homa ndogo.

Majuzi Rais Bolsonaro aliungana na waandamanaji waliokuwa wakipinga marufuku yaliyowekwa na baadhi ya serikali za majimbo nchini humo.

Naye Rais Andry Rajoelina wa Madagascar amezindua dawa ya miti-shamba anayodai inakinga na kuponya corona.

Kinywaji hicho kinatengenezwa kutokana na mmea aina ya Artemisia ambao unatumiwa kutengeneza dawa za kutibu malaria.

Lakini wanasayansi wa mataifa ya magharibi wamepuzilia mbali kinywaji hicho wakisema kinaweza kuwa hatari kwa watumiaji.

Amerika imeathirika zaidi duniani na janga la corona ikiwa na visa zaidi ya elfu 900 vya maambukizi na vifo elfu 52, huku Brazil ikiwa na maambukizi zaidi ya elfu 54 na vifo 3,700.

Tanzania nayo ilikuwa na visa 299 vya maambukizi kufikia jana huku Nairobi ikiongoza maambukizi hapa Kenya.