• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Tutajuta tukipuuza maradhi mengine

TAHARIRI: Tutajuta tukipuuza maradhi mengine

Na MHARIRI

USHAURI unaoendelea kutolewa na wataalamu wa masuala ya afya kuhusu magonjwa yanayoweza kuepukika, unafaa kuchukuliwa kwa uzito na kila mmoja wetu.

Tangu wakati ulimwengu ulipoelekeza macho yake kwa vita dhidi ya virusi vya corona, inahofiwa kuna uwezekano magonjwa mengine hatari yamepuuzwa.

Magonjwa kama vile malaria husababisha vifo vya watu wengi hasa katika nchi za Afrika.

Kando na hayo, iliripotiwa hivi majuzi kuwa baadhi ya watu walioambukizwa HIV wanaogopa kutoka nyumbani, na hivyo hawaendei dawa za kupunguza makali ya maradhi hayo.

Itakuwa ni hatari sana kama wadau katika sekta ya afya na wananchi kwa jumla watazembea kukabiliana na magonjwa aina hiyo wakati huu mataifa yanapopambana na virusi vya corona.

Wakati huu tunapopambana na ugonjwa wa Covid-19, itakuwa hatari sana kama kutatokea mkurupuko wa ugonjwa mwingine katika sehemu yoyote ya nchi.

Itakuwa muhimu serikali kutafuta mbinu ya kuendelea kutoa huduma za afya ya jamii kikamilifu.

Kuna uwezekano wagonjwa wanaamua kujiuguza nyumbani wakihofia kupatikana kuugua virusi vya corona endapo wataende hospitalini.

Inafaa itambulike kuugua corona si tiketi ya moja kwa moja ya kuelekea mautini. Idadi ya waliopona humu nchini kufikia sasa ni kubwa mno ikilinganishwa na waliofariki.

Vilevile, wengi zaidi ya elfu walipatikana hawana ugonjwa huo walipopimwa.

Kwa hivyo ni busara mtu yeyote anayeonyesha dalili za kuugua aende hospitalini ili ibainike kinachomtatiza, na apate matibabu ya haraka.

Inahofiwa pia wengine wanaogopa kwenda hospitalini wakihofia huenda wakambukizwa huko.

Hili ni jambo linalofaa kuangaliwa kwa kina, na wasimamizi wa hospitali wahakikishie umma kuwa kuna mikakati ya kutosha kuepusha maambukizi ya virusi vya corona hospitalini.

Mipango maalumu itahitajika kuwezesha watoto kuendelea kupata chanjo, kwani inahofiwa shughuli hizo zimevurugwa na janga la corona.

Huduma za afya kwa kina mama waja wazito nazo pia ziendelee kutolewa kwa njia salama ili wasihatarishe maisha yao na ya watoto.

You can share this post!

Wanafunzi kukaa nyumbani kwa siku zingine 30

Waasi wa sayansi

adminleo