Michezo

Ligi kuu za Poland, Italia miongoni mwa zinazonukia upya

April 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA

SHIRIKISHO la Soka la Poland limefichua mipango ya kurejelea cha Ligi Kuu ya nchi hiyo almaarufu Ekstraklasa mnamo Mei 29 kwa matarajio ya kuitamatisha rasmi kufikia Julai 19.

Pendekezo hilo limeidhinishwa na Waziri Mkuu wa Poland, Mateusz Morawiecki ambaye ametaka michuano hiyo kusakatiwa katika viwanja vitupu bila mashabiki.

Poland inakuwa nchi ya tano baada ya Ujerumani, Uingereza, Italia na Austria kufichua mipango ya kurejelea ligi kuu za soka katika mataifa yao.

Wiki jana, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson alidokeza uwezekano wa kuanza upya kwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wakati wowote kuanzia Mei 16, 2020.

Tayari vinara wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) wamefichua mipango ya kurejelea kipute hicho mnamo Mei 9 baada ya vikosi vyote 18 vinavyowania ufalme wa msimu huu kukita kambi chini ya mwongozo wa kanuni kali za afya.

Mbali na EPL, ligi nyinginezo ambazo zinatarajiwa kurejelewa chini ya masharti makali nchini Uingereza ni tenisi, kriketi na mbio za farasi.

Hata hivyo, kuanza upya kwa vipute hivi kutakuwa zao la majadiliano ya kina kati ya Baraza la Mawaziri, maafisa wa afya na mashirikisho ya michezo husika nchini Uingereza.

Serikali ya Uingereza inatarajiwa kutoa kauli ya mwisho kuhusu tarehe kamili ya kurejelewa kwa EPL mnamo Mei 7 huku marefa, wachezaji, maafisa na makocha wa vikosi vyote 20 vya ligi hiyo kufanyiwa vipimo vya afya.

Mnamo Aprili 27, wanasoka wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) walitakiwa kurejea kambini kufikia Mei 4 kabla ya vikosi vyote vinavyoshiriki kipute hicho kuanza kujifua rasmi kwa michuano iliyosalia msimu huu mnamo Mei 18, 2020.

Haya ni kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte, ambaye alikariri kuwa “hiyo ni mojawapo ya hatua za awali kabisa zitakazorejesha ukawaida nchini humo kadri wanavyozidi kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona”.

Katika taarifa iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka la Italia (FIGC), kivumbi cha Serie A kimepangiwa kuanza upya wakati wowote kati ya Mei 27 na Juni 2, huku kikitakiwa kutamatika rasmi kufikia mwanzo wa wiki ya kwanza ya Agosti 2020. Mechi 12 zilizosalia katika Serie A muhula huu zitasakatwa ndani ya viwanja vitupu.

Italia ndiyo nchi ambayo imeathiriwa zaidi na virusi vya corona miongoni mwa mataifa yote ya bara Ulaya. Kufikia jana, zaidi ya vifo 26,600 vilikuwa vimeripotiwa nchini humo.

Vifo 260 vilivyotokea mnamo Jumapili ya Aprili 26 ndiyo idadi ndogo zaidi ya watu kuwahi kuaga dunia kutokana na corona nchini Italia tangu Machi 14, 2020.

FIGC tayari imetoa utaratibu utakaoshuhudia wachezaji, makocha, maafisa na wafanyakazi wote katika vikosi vya Serie A wakifanyiwa vipimo vya afya kuanzia Mei 1, 2020.

Kivumbi cha Serie A kiliahirishwa mnamo Machi 9 na wachezaji kadhaa wa ligi hiyo wakapatikana na virusi vya homa kali ya corona.

Beki Daniele Rugani wa Juventus alikuwa mchezaji wa kwanza wa Serie A kupatikana na virusi hivyo kabla ya wanasoka German Pezzella, Patrick Cutrone na Dusan Vlahovic wa Fioretina kuugua ugonjwa huo. Masogora walioathiriwa katika kikosi cha Sampdoria ni Manolo Gabbiadini, Omar Colley, Albin Ekdal, Antonio La Gumina, Morten Thorsby na Fabio Depaoli ambaye aliwaambukiza Blaise Matuidi na Paulo Dybala wa Juventus.

Huku juhudi nyingi zikielekezwa katika kufanikisha mipango ya kurejea kwa Serie A, Massimo Cellino ambaye ni rais wa kikosi cha Brescia kinachovuta mkia jedwalini, ametaka msimu huu mzima wa kipute hicho kufutiliwa mbali na pasiwepo mshindi wala kikosi kitakachoshushwa ngazi. Tukio hilo ndilo lililofanyika katika Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) wiki jana.

Kufikia Jumapili, zaidi ya visa 11,067 vya corona vilikuwa vimeripotiwa nchini Poland ambayo imeshuhudia vifo 499 kutokana na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Marcin Animucki ambaye ni rais wa Ekstraklasa vinara wa soka ya bara Ulaya (Uefa) wamewapendekezea kukamilisha ligi yao kufikia Julai 20.

Amesema kwamba vikosi vitarejea mazoezini kwa makundi mnamo Mei 4 kabla ya wachezaji, marefa na maafisa wote wa benchi za kiufundi kufanyiwa vipimo vya afya kati ya Mei 27-28.

Hadi Ligi Kuu ya Poland ilipoahirishwa mwanzoni mwa Machi 2020 zikisalia mechi 11 pekee kwa msimu kukamilika, Legia na Warsaw walikuwa wakiselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 51 kutokana na mechi 26. Piast Gliwice walikuwa katika nafasi ya tatu kwa alama 43.