Hospitali yajiondolea lawama kifo cha Walibora
Na CHARLES WASONGA
AFISA Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) Dkt Evanson Kamuri amekana madai kuwa wahudumu wa hospitali hiyo walimtelekeza mwandishi mahiri Prof Ken Walibora alipofikishwa huko kwa matibabu Aprili 10.
Dkt Kamuri akihojiwa Jumatatu amewaelezea wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Afya hatua kwa hatua jinsi Profesa Walibora alivyopoteza maisha yake katika hospitali hiyo huku madaktari wakijizatiti kadri wawezavyo kumnusuru.
“Madaktari wetu walijaribu kadri ya uwezo wao kuokoa maisha ya Profesa Walibora lakini kwa bahati mbaya alifariki,” Dkt Kamuri amewaambia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wao Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito kwenye mkutano ulioendeshwa kwa njia ya video ya Zoom.
Kulingana na Dkt Kamuri, Walibora alifikishwa katika KNH na ambulensi ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi saa tatu na dakika 53 asubuhi, Aprili 10, 2020, ambapo alitambuliwa kama Mwanamume Mwafrika asiyejulikana.
“Mgonjwa alikuwa akivuja damu na alikuwa na majeraha mabaya kichwani. Alihudumiwa katika kitengo cha wagonjwa waliojeruhiwa vibaya ambacho kina vifaa sawa na vilivyoko katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU),” ameeleza Dkt Kamuri.
Ameongeza kuwa Profesa Walibora alikaa katika eneo hilo hadi saa kumi za jioni, akihudumiwa, kisha akawekwa katika chumba chenye mitambo ya kumsaidia kupumua.
Dkt Kamuri amewaambia maseneta hao kwamba hali ya marehemu Profesa Walibora ilikuwa mbaya zaidi mwendo wa saa mbili za usiku kutokana na majeraha aliyopata kichwani; hali iliyomfanya kushindwa kupumua.
“Lakini kwa mara nyingine madaktari waliweza kumsaidia akapata uwezo wa kupumua,” ameongeza.
Lakini ilipotimu saa sita na dakika 10 za usiku, Dkt Kamuri amesema, hali ya Walibora ilidhoofika zaidi kutokana na hali kwamba damu iliingia ubongoni mwake.
“Na mwendo wa saa saba na dakika 10, muda wa saa moja baadaye ambapo tulimpoteza,” akasema.
Dkt Kamuri alisema madaktari waliomhudumia Profesa Walibora kwa muda huo wote walikuwa; Dkt Rono, Dkt Sigilai na Dkt Okutoyi.
“Dkt Okutoti ni mtaalamu katika utabibu wa majeraha mabaya, na alisaidiana na wauguzi pamoja na wahudumu wengine wa afya ambao walikuwepo katika Hospitali Kuu ya Kenyatta,” ameeleza alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa maseneta; Fred Outa (Kisumu) na Beth Mugo (Seneta Maalum).
Dkt Kamuri amesema kuwa hospitali ya KNH huwa haibagui wagonjwa na kwamba ilimhudumia Walibora ipasavyo licha ya kwamba hakuwa ametambuliwa rasmi na hakuletwa huko na jamaa zake.
“Kwa hivyo, madai kwamba hospitali hii ilimtelekeza Profesa Walibora sio kweli hata kidogo,” akasisitiza.
“Katika KNH, mgonjwa anapoletwa, huwa hatujali kama una pesa au kadi ya NHIF au hadhi yako katika jamii. Kitu cha kwanza tunachofanya ni kutoa huduma za kwanza za kumtuliza mgonjwa kabla ya kuuliza malipo kwa sababu unaweza tu kulipwa ukiwa hai,” akaongeza.