• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
KAULI YA MATUNDURA: Walibora alivyopagazwa wizi wa miswada

KAULI YA MATUNDURA: Walibora alivyopagazwa wizi wa miswada

Na BITUGI MATUNDURA

MAKALA ya mwandishi Ken Walibora ‘Ukarimu wa Wallah katika tasnia pana ya Kiswahili’ (Taifa Leo, Machi 9, 2017) yaliibua kumbukumbu muhimu katika akili yangu.

Katika makala hayo, Walibora – ambaye nimewahi kudai kuwa ni mmoja wa waandishi aali wa fasihi ya/kwa Kiswahili Afrika ya Mashariki kuwahi kuonekana mpaka sasa, na katika makala yangu – ‘The Power of an enlightened mass’ (Sunday Nation, Agosti 18, 2012) alishangaa ni kwa nini hajashtakiwa kwa ‘wizi wa miswada’. Wala hakuna mtu aliyejitokeza kudai kuwa kaibiwa m(i)swada u/(i)pi, lini na wapi.

Prof Walibora ameukejeli uvumi huu katika riwaya yake – Kidagaa Kimemwozea ambayo niliiandikia tahakiki katika Sunday Nation mwaka wa 2012. Mnamo 2013, mhariri mmoja alinukuliwa akidai kwamba nilikuwa nimemweleza jinsi Prof Walibora alikuwa ‘hodari sana’ katika wizi wa miswada. Taarifa hizo za kusikitisha zilimfikia Prof Walibora – kwa misingi kwamba, katika enzi hii ya utandawazi, taarifa hasa za tetesi husambaa haraka kama moto nyikani wakati wa kiangazi.

Nilijipata babaya – mithili ya panya kwenye kesi ambapo paka ndiye hakimu. Walibora ni msomi ambaye nimekuwa na mlahaka mzuri sana naye tangu mwaka 2003 nilipokutana naye kwa mara ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Nairobi – wakati huo nikihariri habari za Shirika la Habari la Kenya (KBC). Ilisadifu kwamba marehemu Omar Babu – ambaye wakati wa kuzuka kwa porojo hizo alikuwa mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Cologne – Ujerumani, alikuwa rafiki yetu wa karibu – mimi na Walibora.

Marehemu Omar Babu alinitembelea sana – nikawa ninamualika kutoa mihadhara kwa wanafunzi wangu katika Chuo Kikuu cha Chuka ninakofundisha. Kutokana na mtagusano huo, alikuja kufahamu hulka yangu. Kwa hiyo alimpambanulia Prof Walibora kwamba kamwe hadhi na hulka yangu havikuniruhusu kushiriki midahalo hafifu isiyokuwa na msingi kumhusu Prof Walibora kuwapoka watu miswada.

Tetesi kuwa Prof Walibora aliwaperemba watu miswada zinapotazamwa kwa jicho kali, zinakosa mashiko kwa sababu zifuatazo. Kwanza, wanaodai kuibiwa ni akina nani? Pili, mwandishi huyu lazima awe ‘mwizi hodari sana’ wa kuiba miswada zaidi ya 60 (maanake ameandika zaidi ya vitabu 60). Ukisoma kwa makini riwaya ya mtunzi huyu, kuna mtindo unaotawala tungo zake; ‘Siku Njema’ hadi ‘Nasikia Sauti ya Mama’. Kwa kuwa mtindo ni mtu, miswada iliyoibwa haiwezi kuwa na ruwaza ya mtindo fulani unaotawala.

Madai ya wizi wa miswada si jambo geni katika tasnia ya uandishi wa vitabu. Mtu anapotunga kwa kasi inayokiuka ‘uwezo wa binadamu’ wa kawaida, watu bila shaka watamwonea gere. Je, William Shakespeare alitunga tungo zake zote na za viwango vya juu miaka 400 iliyopita? Je, mashairi yaliyopigwa mhuri kuwa ya Muyaka bin Mwinyi yote ni yake au baadhi ni ya Ali Koti?

Prof Walibora amekwisha kufariki. Waliodai kwamba kawaibia miswada walipoteza fursa ya ama kumshtaki mahakamani au kutoa ushahidi wowote mwandishi huyu alipokuwa hai. Kwa hiyo watalazimika kunyamaza milele.

Swali ambalo mwandishi Walibora aliliuliza mara kwa mara ni: “Tunajenga nyumba moja, kwa nini tupiganie fito?” Ni muhimu wakereketwa wote wa Kiswahili watambue kuwa Kiswahili ni bahari kubwa. Sote tunaweza kutoshea katika bahari hiyo – na kila mtu akaogelea kina chake na kwa kasi yake pasi na kuzozana au kuoneana wivu.

 

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

[email protected]

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Kiswahili kitafana iwapo wanahabari...

Mji wa Thika wasafishwa na kunyunyizwa kuepuka Covid-19

adminleo