Matumaini huku waliopona corona wakifika 124
Na VALENTINE OBARA
SERIKALI Jumanne imeendelea kuwapa Wakenya matumaini kwamba taifa litashinda vita dhidi ya virusi vya corona hivi karibuni, baada ya wagonjwa wengine 10 kupona.
Idadi hiyo ilipelekea jumla ya wagonjwa waliopona ugonjwa wa Covid-19 kufika 124.
Ijapokuwa Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman amesema hali hiyo inatia moyo, ameshauri wananchi waendelee kufuata masharti ya serikali kikamilifu kwani bado kuna wengine wanaoambukizwa.
Jumanne, kumekuwa na visa 11 vipya vya maambukizi ambavyo vimetangazwa.
Katika hotuba ya serikali ya kila siku kuhusu hali ya coronavirus nchini, Dkt Aman amesema jumla ya maambukizi sasa ni 374.
Wagonjwa waliotangazwa Jumanne wamejumuisha watoto wawili wenye umri wa miaka mitatu, huku mgonjwa aliye na umri mkubwa zaidi akiwa ni wa miaka 75.
Miongoni mwa hao 11, saba walipatikana Nairobi huku wanne wakitoka Mombasa.
Dkt Aman amesema wale walio Nairobi wametoka mitaa ya Kawangware (wanne), Eastleigh, Manji Estate na Kaloleni.
Wa Mombasa wote walikuwa kutoka mtaa wa Kibokoni. Hii imefanya idadi ya wagonjwa waliopatikana Nairobi kufika 241, na Mombasa 97.
“Kwa siku chache sasa tumetambua maambukizi yanaenea Nairobi na Mombasa. Tumeanza mipango ya kudhibiti zaidi ueneaji virusi katika kaunti hizo mbili. Tunaomba kaunti nyingine zote ziendelee kuwa macho,” amesema.
Ametoa wito kwa kikosi cha polisi kiendelee kujitahidi kuhakikisha watu hawaingii wala kutoka katika kaunti hizo, ili kuzuia ueneaji wa virusi vya corona kwa kaunti nyinginezo.