• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 2:10 PM
Familia Limuru yabaguliwa ghafla kushukiwa corona

Familia Limuru yabaguliwa ghafla kushukiwa corona

Na MARY WANGARI

FAMILIA moja eneo la Limuru, Kaunti ya Kiambu sasa inataka serikali iwachukulie hatua walioeneza video na habari mitandaoni inazosema ni za uongo, kuhusu mazishi ya jamaa yao aliyeshukiwa kuwa na Covid-19.

Hii ni baada ya familia hiyo pamoja na majirani waliokuwa wakiishi jengo moja na marehemu kujipata wakiwa wametengwa ghafla na wakazi kwa kushukiwa kuambukizwa maradhi hayo hatari.

Masaibu ya familia hiyo yalianza baada ya mwendazake, Bw David Kamau, almaarufu DJ Davy Younster mwenye umri wa miaka 22, kufariki katika hospitali ya Kiambu Level 5 kutokana na maradhi ya pumu.

Kulingana na kaka ya marehemu, mwendazake alikuwa amelalamika kuhusu maumivu ya kifua ambayo ni dalili mojawapo ya virusi vya corona kabla ya kufariki hospitalini na kuzikwa kuambatana na utaratibu wa Wizara ya Afya.

“Kwa sababu ya tahadhari, maafisa wa afya walitueleza kuwa atazikwa kama mgonjwa wa Corona hata ikiwa hatukuwa na hakika kabla ya matokeo ya kubaini kiini cha kifo chake kutolewa. Matokeo ya vipimo hutolewa baadaye,” alieleza kaka yake marehemu.

Hata kabla ya familia hiyo kupata muda wa kumwomboleza mpendwa wao, ilijipata ikiwa imetengwa ghafla pamoja na majirani waliokuwa wakiishi jengo moja na mwendazake kufuatia video kuhusu mazishi hayo eneo la Nyambari, kusambazwa mno mitandaoni.

Katika video hiyo, jeneza la marehemu lilionekana likiwa limefunikwa karatasi nyeusi huku maafisa wa afya waliomzika wakiwa wamevalia magwanda kamili ya kujikinga pamoja na vijichupa vya dawa ya kuua viini.

Video hiyo ilienezwa mno mitandaoni kuanzia Jumanne hadi Jumatano kabla ya matokeo ya vipimo kutangazwa, ambapo wahusika waliitumia kama onyo kuhusu Covid-19 na kuwaacha wakazi wakihofia maisha yao.

“Sasa watu wote wametutenga kwa kudhani kwamba mwanangu alifariki kutokana na corona na hata hawana hakika kwa kuwa mimi nasubiri matokeo ili nijue ikiwa ni corona au la. Ikiwa alikuwa na virusi hivyo, si hata sisi basi tumeambukizwa,” alieleza mamake marehemu

Licha ya wakazi kushusha pumzi baada ya matokeo kuthibitisha hakikiwa kisa cha Covid-19, athari kisaikolojia iliyosababishiwa familia ya mwendazake ikiwemo majirani haielezeki kutokana na walioeneza uvumi huo mitandaoni.

“Sisi kama familia hatukufurahsihwa na tukio hilo. Shauku letu lilikuwa kumuaga mpendwa wetu kwa heshima inayostahiki kwa sababu alikuwa mtu aliyependwa na watu,” alisema kaka yake marehemu.

Hii ni kwa kuzingatia sheria inayopiga marufuku uenezaji wa habari zozote za uongo kuhusiana na mkurupuko wa Covid-19 na kusababisha taharuki miongoni mwa watu.

“Nani anamjua? Ndiye aliyeanzisha uvumi huo uliosababisha unyanyapaa dhidi ya familia yangu. Mtu amshauri kwa sababu serikali imepiga marufuku habari kama hizo,” alieleza Rachel Karihe.

“Ushauri wa kisheria kwa familia, mnapaswa kuwashtaki wasimamizi wa kurasa za mtandao kwa kuruhusu tetesi kama hizo za kizushi kuhusu kifo chake. Hivyo tu,” Caleb alishauri.

Tukio hilo limejiri huku visa vya unyanyapaa dhidi ya wahasiriwa wa Covid-19 vikiongeza kwa kasi na kutishia kuhujumu juhudi za serikali za kudhibiti janga la hilo la kiafya ambalo limetikisa ulimwengu wote.

Akizungumza na vyombo vya habari, Chifu wa eneo la Limuru, Francis Kimani aliwatahadharisha wakazi dhidi ya kueneza habari za uongo na unyanyapaa dhidi ya wahasiriwa.

You can share this post!

‘Meme Lord’ asimulia alivyojinasia penzi...

Anayetakiwa Afrika Kusini kwa utekaji nyara aachiliwa huru

adminleo