UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Alama ya kistari kirefu, au deshi (-) katika uakifishaji
Na MARY WANGARI
KATIKA Makala ya leo, tutajadili na kujifahamisha zaidi kuhusu matumizi ya kituo cha deshi au ukipenda kistari kirefu katika uakifishaji.
Jinsi ya kutumia kituo cha deshi
Alama ya deshi hutumiwa kama kiunganishi cha sentensi mbili iwapo sentensi ya pili inafafanua sentensi ile ya kwanza. Mathalan:
Uzuri wa mwanamke ni tabia – unyenyekevu na heshima.
Wachezaji machachari – Kamau, Njenga, Zawadi na Nyota – walituzwa zawadi.
Alama ya deshi hutumika sawa na jinsi kituo cha parandesi kinavyotumika kwa madhumuni ya kuongeza maelezo au taarifa zaidi kuhusu neno, sentensi au usemi uliotangulia.
Matumizi sahihi yanahusisha alama mbili za deshi ambapo deshi ya kwanza hutumika kwenye mwanzo wa maelezo ya ziada na hiyo nyingine mwishoni mwa maelezo hayo ikiwa yamo katikati mwa sentensi. Kwa mfano
Mikakati iliyowekwa na serikali ya Kenya – kupiga marufuku mikusanyiko ya watu, kutangaza kafyu, kuwaagiza wananchi kuvalia maski na kadhalika – imechangia pakubwa kudhibiti maabukizi ya Covid-19 nchini.
Mwalimu wangu – wa Fizikia – alifanya nipende na kupasi somo hilo.
Alipofika tu alikimbia kumpasha habari hizo – kumbe tayari alikuwa amejua ukweli.
Kituo cha deshi pia hutumiwa badala ya alama ya nuktapacha katika mazungumzo hasa mahojiano. Kwa mfano.
Mhojaji – Ulianza kuimba lini? Nini kilichokupa mshawasha wa kujitosa katika tasnia ya muziki?
Mhojiwa – Tangu nikiwa mdogo nilikuwa ninapenda kuimba na niligundua nina talanta ya uimbaji nikiwa na umri mchanga sana. Baba yangu alikuwa mwimbaji maarufu wa taarabu na ndiye aliyenipa motisha ya kuanza kutunga na kuimba vilevile.
Aidha, badala ya kutumia alama ya koloni, kituo cha deshi hutumiwa kuorodhesha mambo. Kwa mfano:
Alama ya kistari kirefu hutumiwa kuandika orodha. Mathalan
Fasihi andishi ina tanzu kadhaa – ushairi, riwaya, hadithi fupi tamthilia
Mazishi ya Rais Mstaafu Daniel Arap Moi yalihudhuriwa na watu wa aina yote – wazee, vijana, wanawake wanaume na watoto.
Badala ya:
Mazishi ya Rais Mstaafu Daniel Arap Moi yalihudhuriwa na watu wa aina yote: wazee, vijana, wanawake, wanaume na watoto
Wasiliana na mwandishi kupitia baruapepe: [email protected]
Marejeo
Mkinga, M.G. (2007). Kiswahili kwa Shule za Msingi 2 (MWL), Dar es Salaam: Educational Books Publishers Ltd.
Norton, S. & Green, B. (2002). Essay Essentials with Reading, Tol. 3, Edinburgh: Thomson Nelson.
Stephano, R. (2015). “Uzingatizi wa Viakifishi katika Uandishi wa Kitaaluma: Mifano kutoka Shule za Msingi Tanzania.” Tasnifu ya Shahada ya Uzamivu ya Chuo Kikuu cha Dodoma (haijachapishwa).