UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kituo cha kistari kirefu, deshi (-) katika uakifishaji
Na MARY WANGARI
KATIKA makala ya leo, tutaendelea kujifahamisha kuhusu kituo cha deshi katika uakifishaji na jinsi matumizi yake sahihi katika uandishi.
Matumizi ya kistari kifupi, deshi
Alama ya deshi hutumiwa kuonyesha jina la msemaji au mwandishi ambaye usemi dondoo au kitabu chake kimekaririwa.
Kwa kawaida, matumizi sahihi ni kwamba kituo cha deshi huandikwa mbele ya jina la mwandishi, msemaji au mhusika.
“Ukiwa na fedha utajuta, ukiwa huna utajuta. Cha nini kitu kama hiki!”
(Utubora Mkulima – Shaaban Robert).
Alama ya deshi pia hutumiwa kuonyesha maneno yaliyosemwa lakini hayakukamilika.
Mathalani katika mazungumzo, maelezo, mahojiano, na kadhalika. Kwa mfano:
Mtangazaji – Unafikiri janga la virusi vya corona litatuondokea hivi karibuni?
Rais – Kwa kweli siwezi kusema kwa hakika ila cha muhimu ni kuwa na matumaini kwamba hali itaimarika huku wanasayansi wetu wakizidi kutafuta tiba ya gonjwa hilo.
Mzazi – Usichelewe
Mtoto – Nitafika mapema
Kituo cha deshi pia hutumiwa badala ya alama ya mkato katika uakifishaji ili kuonyesha maelezo au taarifa za ziada katika sentensi au usemi. Kwa mfano:
Ni muhimu tuzingatie masharti yote – ndiyo namna pekee ya kujikinga- ili tuweze kuzuia maambukizi zaidi ya Covid-19,
Badala ya kutumia kituo cha koma jinsi ifuatavyo:
Ni muhimu tuzingatie masharti yote, ndiyo namna pekee ya kujikinga, ili tuweze kuzuia maambukizi zaidi ya Covid-19.
Kituo cha deshi vilevile hutumiwa kuorodhesha mambo kadhaa yanayofuatwa na maelezo ya ziada. Kwa mfano:
Mafuriko, maporomoko ya ardhi, uvamizi wa nzige wa jangwani, na sasa janga la Covid-19 – ni dhahiri kwamba 2020 umekuwa mwaka mgumu si haba.
Amerika, Italia, Uingereza – ni miongoni mwa mataifa ya Magharibi yaliyoathiriwa zaidi na janga hilo la kiafya.
Alama ya deshi pia hutumiwa kuonyesha msisitizo au mkazo katika usemi. Kwa mfano:
Ni sharti tukumbuke jambo moja – hakuna binadamu aliye mkamilifu
Licha ya yote yanayotendeka ukweli ni kuwa – hakuna asiyependa kupendwa.
Tahadhari unapotumia kistari kirefu katika uakifishaji
Hata hivyo, ili kutumia alama hizi za uakifishaji kwa njia sahihi, ni muhimu kuelewa kwamba kituo cha deshi na alama za mnukuu huwa hazitumiki kwa pamoja.
Aghalabu mara nyingi alama ya deshi inapotumika, alama za kunukuu hazitumiki na vinginevyo.
Wasiliana na mwandishi kupitia baruapepe: [email protected]
Marejeo
Leech, G. (1983). Principles of Pragmatics. London: Longman.
Makombo, H. & Wachira, W. (2008). Misingi ya Kiswahili 4 (MWF). Dar es Salaam: Ujuzi Books Ltd.
Masood, A. J. (2013). Kiswahili kwa Shule za Msingi 3 (MWL), Dar es Salaam: Educational Books Publishers Ltd.