Jagina wa Gor afariki, mazishi ni Jumanne
Na CECIL ODONGO
JAGINA wa Gor Mahia Martin Ouma ‘Ogwanjo’ ambaye aliaga dunia mnamo Jumamosi asubuhi akiwa na umri wa miaka 71, atazikwa mnamo Jumanne nyumbani kwake kijiji cha Hawinga, eneobunge la Alego Usonga, Kaunti ya Siaya.
Kulingana na mwanawe Tom Ouma, marehemu aliaga dunia baada ya kuugua kiharusi na mwili wake ukapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Bama mjini Siaya.
“Babangu amekuwa akiugua kiharusi kwa muda wa miaka mitatu iliyopita. Alianguka na kuaga dunia akiwa nyumbani. Mipango ya mazishi inaendelea na atafukiwa mchangani mnamo Jumanne inshallah,” Tom akaeleza ‘Taifa Leo’.
Ouma atakumbukwa kwa kuongoza Gor Mahia kufika fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika (CAF winners cup) mnamo 1979 ambapo walipoteza 2-0 nyumbani na 4-0 ugenini.
Aliongoza Gor Mahia kushinda taji la Ligi Kuu (KPL) bila kushindwa mnamo 1976.
Pia alikuwa kati ya wachezaji walioshiriki Kombe la Taifa Bingwa Afrika na timu ya taifa Harambee Stars mnamo 1972.
Nahodha wa kikosi cha Gor Mahia kilichoshinda Kombe la Mandela Barani Afrika mnamo 1987, Austin Oduor ‘Makamu’ alisema Ouma ambaye walikuwa naye kwenye kikosi cha 1980, alikuwa mchezaji mahiri ambaye alijituma sana akiwa uwanjani kuhakikisha timu yake inapata ushindi.
“Alikuwa mchezaji aliyejaliwa talanta ya kuwachenga madifenda na kutoa pasi za uhakika. Wao ndio walivumisha Gor enzi hizo wakiwa na rafiki yangu Allan Thigo. Kando na kucheza naye kabla aondoke Gor mwisho wa msimu wa 1980, nilicheza dhidi yake akiwa K’Ogalo nami nikiwa Luo Stars 1978,” akasema Oduor.
Akaongeza: “Nilikutana naye mara ya mwisho mnamo 2017 uga wa Kasarani tulipoalikwa kama majagina kutazama debi ya Mashemeji.”
Kutokana na agizo la serikali inayopiga marufuku mikusanyiko ya watu katika maeneo ya umma kutokana na virusi vya corona, ni familia yake na jamaa wachache watakaohudhuria maziko yake.