Simbas watoa mwongozo mpya wa kuboresha raga nchini Kenya
Na CHRIS ADUNGO
BENCHI ya kiufundi ya kikosi cha raga ya wachezaji 15 kila upande, Simbas, imebuni mwongozo mpya wa ukufunzi na usimamizi utakaosaidia pia klabu mbalimbali kujiimarisha na kuboresha maandalizi yao baada ya shughuli za michezo kurejelewa.
Michezo yote kwa sasa imesitishwa humu nchini na katika mataifa mengi duniani kote kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.
Mwongozo huo unashughulikia masuala ya afya, jinsi ya kuimarisha mazoezi ya viungo vya mwili miongoni mwa wanaraga na namna ya kuboresha idara za ulinzi, kati na uvamizi za vikosi. Mwongozo huo unapania pia kuwapa maafisa wa mechi mbinu bora zaidi za kukumbatia kila wanaposimamia au kuendesha michuano mbalimbali.
Kocha Paul Odera amekiri kwamba analenga kuutumia mwongozo huo kwa kipindi chote kilichosalia katika mkataba wake na kikosi cha Simbas na kile cha wanaraga chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, Chipu.
“Tutakuwa tukifanyia mwongozo huo mabadiliko ya mara kwa mara ili uwiane na mazingira na mahitaji yote ya raga ya humu nchini pamoja na viwango vya kimataifa,” akasema Odera.
Mwanaraga huyo wa zamani wa timu ya taifa ya wachezaji saba kila upande, Shujaa, amesema vikosi vya Kenya vinakosa mtindo ambao ni kitambulisho chao katika ulingo wa raga ikilinganishwa na Afrika Kusini, New Zealand, Uingereza, Australia na Ufaransa ambao ni miamba wa mchezo huo duniani.
“Mfumo na mtindo wetu wa kucheza unastahili kujumuisha upana wa utamaduni wetu bila ya yeyote kubaguliwa kwa misingi ya rangi, kabila au mahusiano ya kijamii. Uwezo wa wanaraga wetu kutumia uchache wa raslimali tulizonazo na kuchuma nafuu kutokana na vipaji vya mbio na ukubwa wa miili unastahili kuwa kitambulisho chetu,” akaongeza.
Simbas walikuwa wameanza kujifua mapema Machi 2020 kwa minajili ya kampeni mbalimbali za raga ya kimataifa kabla ya Serikali kusimamisha kwa muda michezo yote kutokana na janga la corona ambalo limetikisa ulimwengu mzima.
Chini ya Odera, kikosi cha Simbas kilikuwa kimepangiwa kuchuana na Morocco, Uganda na Zimbabwe katika kipute cha kuwania ufalme wa Raga ya Bara la Afrika mwishoni mwa Mei kabla ya kinyang’anyiro hicho kuahirishwa.
Simbas walikuwa pua na mdomo kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za Raga mnamo 2015 kabla ya kuzidiwa maarifa na Namibia.
Katika makala ya Raga ya Afrika mwaka jana, Simbas waliambulia nafasi ya pili nyuma ya Namibia barani kabla ya kupepetwa na Canada, Hong Kong na Ujerumani katika kundi la kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Chipu nao walikuwa wakijifua kwa minajili ya kipute cha Barthes Cup kilichotarajiwa kuandaliwa jijini Nairobi mnamo kati ya Aprili 19-22. Odera aliwahi kukiri kwamba changamoto kubwa anayokabiliana nayo kambini mwa Chipu ni ugumu wa kuoanisha mitindo ya kucheza kwa wanaraga wake.
Hilo lilichochea Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) kujinasia huduma za wakufunzi Hans Joubert na Neil De Kock kutoka Afrika Kusini mnamo Februari 2020. Wawili hao walikuwa washirikiane na Odera kuwanoa wanaraga wa Chipu kwa minajili ya kutetea ubingwa wa Barthes Cup mnamo Aprili 2020.
Kenya ilitazamia kutumia mashindano hayo kufuzu kwa Raga ya Dunia kwa Chipukizi (JWRT) nchini Uhispania mnamo 2020 na fainali za Kombe la Dunia nchini Ufaransa mnamo 2023.