Kuna uhaba mkubwa wa damu nchini
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya walipigwa na butwaa Jumatatu walipofahamishwa kuwa Kenya haina hifadhi ya damu, ishara kwamba wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu wanataabika.
Katika ripoti iliwasilishwa mbele ya kamati hiyo na jopo lilloteuliwa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kuchunguza usambazaji na matumizi ya damu nchini, hamna hata tone ya bidhaa hiyo katika hifadhi za Nairobi na Mombasa kati ya maeneo mengine yanayosimamiwa na Shirika la Kitaifa la Damu (KNBTS).
Mwenyekiti wa jopo hilo Abbas Gullet aliambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a Sabina Chege kwamba KNBTS inakabiliwa na changamoto ya usimamizi mbaya, utepetevu wa wafanyakazi na ukosefu wa fedha za kuendesha shughuli zake.
“Wafanyakazi hawana motisha ya kazi, hawana vifaa vya kazi. Tulipokuwa huko wiki jana tuliarifiwa kuwa hata kipimo kimoja cha damu hakiwezi kupatikana,” akasema.
Akaongeza: “Kama Wakenya tulishangazwa sana na yale tuliona na inamaanisha kuwa tuna kibarua kikubwa. Ukweli ni kwamba KNBTS inakabiliwa na changamoto kubwa ambayo isiposhughulikiwa tutatumbukia katika shida kubwa.”
Bw Abbas majuzi pia aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Shirika hilo. Hii ni baada ya kustaafu wadhifa wake wa zamani wa Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Nchini.
Jopo hilo ambalo linashirikikisha wawakilishi kutoka vitengo mbalimbali vya kitaalauma lilikuwa likitoa maoni yake kwa Mswada unaolenga kuboresha shughuli za upeanaji damu nchini.
Wanachama wengine wa jopo hilo lenye wajibu wa kutoa ushauri kuhusu suala hilo ni; Dkt Peter Kibet Shikuku, Dkt Elizabeth Wala Bharat Thakrar, Dkt Patrick Murugami, Profesa Bitange Ndemo na Joe Wang’endo.
Nao wengine Charles Rombo, Kiprono Chepkok na Dkt Thuranira Kaugiria na makatibu wenzao wa jopo hilo.
“Kwa sababu tulipotembelea hifadhi ya damu hatukupata kipimo chochote cha damu, dharura ikitokea ambapo damu inahitaji haraka, usaidizi hauwezi kupatikana,” akasema Bi Wang’endo.
Mwaka 2019 Kenya ilikusanya vipimo 164,000 vya damu ilhali lengo lilikuwa ni vipimo 500,000.
Hii ina maana kuwa Kenya ilikusanya thuluthi moja pekee ya hitaji jumla la damu kwa mwaka mmoja.
Mswada huo pia unalenga kuhakikisha kuwa KNBTS inatoa huduma sawa bila ubaguzi.
Malalamiko
Malalamishi yamekuwepo kwamba shirika hilo huwahudumia watu matajiri pekee huku watu wengi wasio na uwezo wa kifedha wakiachwa kufariki kwa ukosefu wa damu.
Vilevile, mswada huo utaunda mwongozo wa utekelezaji wa sera na viwango vya kuhakikisha kuwa dawa inayopewa wagonjwa ni salama.
“Mswada hu pia unalenga kuweka mwongozo thabiti wa kuziba mianya ambayo imekuwa ikifanikisha wizi wa damu,” Bi Chege anasema kwenye taarifa inayoelezea malengo ya sheria hiyo kielelezo.
Katika miaka ya hivi karibuni kumeibuka ripoti za uuzaji damu katika mataifa jirani kinyume cha sheria.
Na watuhumiwa katika uovu huu wamekuwa ni wafanyakazi wa shirika lili hili la KNBTS wakishirikiana na wahudumu wengine wa afya.
Kwa mfano, mnamo Oktoba mwaka jana, mhudumu mmoja wa afya mjini Kisumu alihudumiwa kortini kwa kosa la kupokea hongo ya Sh28,000 ili auzie mgonjwa fulani damu.
“Mtu yeyote ambaye atakusanya, kutoa, kusambaza na kushiriki biashara ya damu au bidhaa za damu kinyume na sheria hii atakuwa ametenda kosa. Na mtu kama huyo ataadhibiwa kwa faini isiyozidi Sh1 milioni au kifungo kisichozidi miaka mitatu gerezani au adhabu zote mbili,” mswada huo uliochapishwa Machi unasema.
Mswada huo ukitiwa saini kuwa sheria serikali za kaunti zitahitajika kufanya kazi kwa ushirikiano na KNBTS kuhakikisha viwango vya usalama wa damu vinazingatiwa.