Golikipa wa Gor Mahia ataka mshahara wake la sivyo hatorejea nchini
Na CECIL ODONGO
MNYAKAJI wa Gor Mahia David Mapigano ameueleza uongozi wa timu hiyo umlipe malimbikizi ya mshahara wake la sivyo hatarejea nchini kuwasakatia mabingwa hao mara 19 wa Ligi Kuu (KPL).
Mwanadimba huyo raia wa Tanzania pia ameueleza uongozi wa K’Ogalo kwamba hatashiriki kwenye mazungumzo yoyote wa kurefusha kandarasi yake hadi alipwe fedha zake.
Mapigano alisajiliwa na K’Ogalo kutoka Singida United mnamo Julai 2017 kwa mkataba wa miaka mitatu ambao unatarajiwa utakamilika mnamo Julai 2021.
K’Ogalo bado haijawalipa wachezaji wake mishahara kwa miezi saba iliyopita, hali hii ikisababishwa na ukosefu wa mdhamini baada ya kuondoka kwa Sportpesa mnamo Agosti mwaka jana.
“Sitarejea Kenya kuendelea kuichezea Gor Mahia kama hawatakuwa wamenilipa mishahara ninayowadai. Nimewapa muda wanilipe na hilo lisipowezekana, basi familia yangu imenikubalia nisalie huku,” akasema Mapigano kwenye mahojiano na Taifa Leo kutoka jiji la Arusha.
Aidha alifichua kwamba amepokea ofa nyingi kutoka kwa timu za Tanzania na kutoka nchi nyingine, ndiyo maana hatasita kujiunga na moja kati yao iwapo Gor watakosa kumlipa fedha zake.
“Ni kweli timu nyingi zinawania huduma zangu kama mpira wa kona. Hata hivyo, nimeziambia zisubiri nikiwa na matumaini Gor watawajibika na kunipokeza hela zangu. Nitaandika barua ya kutamatisha kandarasi yangu kama hali haitabadilika,
“Napenda Gor ndiyo maana nimekuwa mvumilivu lakini subira hiyo ikikosa kuvuta heri, basi sitakuwa na jingine ila kuondoka,” akaongeza Mapigano.
Kipa huyo wa Taifa Stars pia aliwapongeza wachezaji wenzake kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu (KPL) kwa mwaka wa nne mfululizo.
Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Nick Mwendwa Alhamisi wiki jana, alitangaza Gor bingwa wa msimu huu na ilifikisha jina la K’Ogalo kama mwakilishi wa Kenya kwenye mechi za Klabu bingwa Afrika msimu ujao.
Mechi za KPL zilisitishwa kutokana na janga la corona mnamo Machi. Mitanange 10 ilikuwa imesalia ili msimu wote utamatike.
Hata hivyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa KPL Jack Oguda amepinga kutawazwa kwa K’Ogalo, akisema mustakabali wa msimu huu utaamuliwa baada ya kukamilika kwa siku 21 za kafyu mnamo Mei 15.
“Iwapo kuna sheria ambazo zinatupokeza ubingwa basi ni sawa. Hata hivyo, ingekuwa bora iwapo tungeshinda taji kwa kuwajibika uwanjani. Hatukuwa tayari kuona msimu huu ukitamatika ghafla,” akaongeza Mapigano.
Iwapo ataondoka, K’Ogalo sasa itasalia na wanyakaji Boniface Oluoch na Fredrick Odhiambo.