Makala

MASAIBU: Ubomoaji waathiri vibaya wakazi wa Korogocho

May 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

SIKU moja tu baada ya wakazi wa mtaa wa mabanda wa Kariobangi Sewage kuachwa bila makao na wengi kukesha nje kufuatia ubomoaji uliofanywa Jumatatu, wafanyabiashara 500 katika soko jirani la Korogocho hawakuwa na lao shughuli hiyo ilipoendelea hadi katika biashara zao Jumanne.

Katika siku ya kwanza ya ubomoaji huo wa kuondoa watu waliojenga nyumba katika ardhi karibu na sehemu ya kusafisha majitaka ya Kariobangi, zaidi ya watu 12,000 waliachwa bila makao.

Matingatinga manne yalifika katika mtaa wa mabanda wa Kariobangi Sewage na kubomoa kabisa eneo hilo, licha ya kuwa mahakama ilikuwa imetoa agizo shughuli hiyo isimamishwe hadi kesi iliyowasilishwa na wakazi hao isikizwe na kuamuliwa hapo Mei 7.

Chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi, matingatinga hayo yalibomoa mtaa huo kabla ya kuingilia soko mapema Jumanne.

Watu wengi walioachwa bila makao bado walikuwa wanasafirisha mali yao hapo Jumanne.

Mnamo Jumatatu, baadhi walitafuta hifadhi katika makanisa na wengine wakalala kwenye veranda katika mtaa jirani wa viwandani wa Kariobangi Industries.

Mwathiriwa wa ubomoaji wa mtaa wa mabanda wa Kariobangi Sewage atafuta hifadhi kwenye veranda Kariobangi industries. Picha/ Geoffrey Anene

Hata hivyo, mamia ya watu kutoka mtaa wa Kariobangi Sewage waliokosa kabisa pa kuenda, walikesha kwenye baridi kali wakilala kwenye viti vyao.

“Mimi nililala hapa nje kwa sababu sina mahali pa kuenda wala fedha za kutafuta makao mengine,” ajuza mmoja aliambia tovuti ya Taifa Leo katika mahojiano na kufichua kuwa hajawahi kupata malipo ya watu wazee kutoka kwa serikali, licha ya kuwasilisha jina kwa chifu inavyohitajika.

Hapo Jumanne, wauzaji wa bidhaa mbalimbali walibomolewa vibanda vyao.

Wengi waliobomolewa vibanda walikuwa katika upande wa mkono wa kushoto unapoingia soko la Korogocho ukitokea barabara ya Komorock, ambayo pia iliendelea kushuhudia msongamano mkubwa wa magari kwa siku ya pili mfululizo.

Mfanyabiashara mmoja alieleza tovuti hii kuwa hawakuwa wamepata notisi ya kuondoka.

“Tulidhani shughuli ya ubomoaji inbgfanyika tu katika sehemu ambayo watu waliishi. Hatukujua kuwa pia sisi tulifaa kuondoa vibanda vyetu,” alisema, huku akifichua kuwa kuna wafanyabiashara walio na vibanda vyao na kuna wengine ambao hukodisha vibanda na kuvilipia Sh3,000 kila mwezi.

Kubomolewa kwa makao hayo hata hivyo kumefungua biashara nyingine za uuzaji wa mabati na kuni.

Mfanyabiashara mmoja wa kuuza mabati alisema bati moja sasa linanunuliwa kwa Sh11.00. Hata hivyo, kuna sehemu, ambazo bati moja lilikuwa likiuzwa kwa Sh350. Watu bado wanahama eneo hilo.

Biashara ya mabati imenoga baada ya mtaa wa mabanda wa Kariobangi Sewage kubomolewa. Picha/ Geoffrey Anene

Kuna ubomoaji wa sehemu ya juu ya mtaa wa Korogocho uliofanywa Jumanne, kitu ambacho sasa kimetia wakazi wasiwasi.

Wengi sasa wanaomba serikali iondoe marafuku waliyowekewa wakazi wa Nairobi kwa sababu ya janga la Covid-19 ili wasafiri mashambani.

Ubomoaji wa Jumanne ulishuhudia barabara ya kuingia Korogocho ikichimbwa mtaro na majitaka kuelekezwa kwenye Mto Nairobi.