Usimamizi wa Tusker sasa unakarabati uwanja wao wa Ruaraka
Na CHRIS ADUNGO
WASIMAMIZI wa kikosi cha Tusker FC wameanza kuukarabati uwanja wao wa nyumbani wa Ruaraka baada ya soka ya humu nchini kusitishwa kutokana na janga la corona.
Vinara wa mabingwa hao mara 11 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) wamethibitisha kwamba kwa sasa wanawekea uwanja wa Ruaraka zulia jipya.
Isitoshe, mwenyekiti wao Daniel Aduda amesema kwamba wanashughulikia pia mifereji ya majitaka katika jitihada za kurejesha hadhi ya uwanja huo ambao umekuwa katika hali mbaya kwa kipindi kirefu.
“Licha ya uchechefu wa fedha unaotukabili, kikosi kimepania kuchuma nafuu kutokana na janga hili na kukarabati uwanja chini ya uelekezi wa Wycliffe Omondi anayesimamia masuala ya uga wa Ruaraka,” akasema Aduda.
Vinara wa Tusker na wa Kamati ya KPL ya Viwanja na Usalama wamekuwa wakikashifiwa pakubwa kwa kuidhinisha mechi mbalimbali kusakatiwa ugani Ruaraka licha ya hali duni ya uwanja huo.
Mbali na kutumiwa kuandalia michuano mbalimbali ya KPL, uwanja wa Ruaraka umekuwa pia mwenyeji wa mapambano ya Ligi ya Kitaifa ya Daraja ya Kwanza (NSL) na gozi la Betway Shield Cup msimu huu.
“Uwanja wa Ruaraka umekuwa ukitumika zaidi kabla ya mlipuko wa virusi vya corona kutokea. Tulifanyia mazoezi hapa na pia kuchezea mechi zetu zote za nyumbani ugani humu. Kutokuwepo kwa mvua kwa siku kadhaa zilizopita kumetupigisha hatua zaidi chini ya usimamizi wa Omondi. Sasa kukashifiwa na kushtumiwa kwingi kutakwisha,” akasema Aduda.
Baada ya uwanja huo kukarabatiwa, ipo mipango ya shughuli za ujenzi wa maeneo ya wageni rasmi na mashabiki pia kukalia. Hili ni jambo ambalo Aduda ameshikilia kwamba litaupa uga wa Ruaraka sura mpya kwa mujibu wa viwango vya ubora vinavyohitajika.
Kinara huyo pia amesisitiza kwamba Tusker hawaungi mkono wala kupinga upande wowote katika vita vya ubabe kati ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) na waendeshaji wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL).
Vita baina ya wadau hao wa soka ya humu nchini vilizuka wiki iliyopita baada ya Rais wa FKF, Nick Mwendwa kutamatisha rasmi kampeni za msimu huu na kutawaza Gor Mahia na Nairobi City Stars kuwa washindi wa KPL na NSL mtawalia.
Kwa pamoja na Kakamega Homeboyz walioambulia nafasi ya pili, Tusker walikuwa pia katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa KPL msimu huu hasa ikizingatiwa pengo la alama nane pekee kati yao na Gor Mahia waliokuwa wamesakata mchuano mmoja zaidi kuliko wao hadi kipute cha KPL kilipositishwa mwanzoni mwa Machi 2020.
Ingawa hivyo, Aduda amewasihi vinara wa FKF na KPL kuafikiana haraka iwezekanavyo na kutoa mwongozo utakaoheshimiwa na washiriki wote wa kampeni mbalimbali za soka ya humu nchini.