• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
SANAA: Anaimairisha viatu kwa ubora na mwonekano aupendao mteja

SANAA: Anaimairisha viatu kwa ubora na mwonekano aupendao mteja

Na MARGARET MAINA

[email protected]

NILIBAINI wapo watu wengi sana ambao hununua vitu sawa kwa wakati mmoja na ndipo nikajiuliza, ikiwa watu 500 wana jozi moja ya viatu, ninaweza kufanya nini kubadili mwonekano wao?

Hili ndilo swali ambalo lilikuwa katika akili ya Westbury Ngigi, 21, ambaye alianzisha kazi ya sanaa kwa madhumuni ya kuimarisha viatu kwa ubora na mwonekano ili kuafiki matakwa ya mteja wake.

Anafanya hivyo kwa kuongeza nakshi na madoido akitumia rangi mbalimbali.

Mwanafunzi huyu wa shahada ya sanaa katika Chuo Kikuu cha Unicaf ambaye ni mkaazi wa Thika, alianzisha biashara yake hii mnamo Septemba 2019 kwa kutumia talanta yake ya sanaa ili kupata pesa za kugharimia mahitaji yake ya kila siku. Alianzisha biashara hii kwa mtaji wa Sh3,600 alizopewa na baba yake.

“Nilianza sanaa nilipokuwa mdogo na nilipata shida na mara kwa mara iliniingiza katika hali ya mvutano baina yangu na walimu kwa sababu nilikuwa nikichora picha za vibonzo hata kwenye vitabu vya shule yangu. Ingawa hivyo, wazazi wangu waligundua nilikuwa na talanta,” anasema.

Ngigi alijifunza biashara hii kutoka kwa Youtuber Maxine Wabosha ambaye aliwahi kufanya video kuhusu jinsi ya kubadilisha viatu vya Rubber.

“Ninatumia rangi na brashi kupamba viatu. Kununua rangi kunanigharimu Sh 800 kwa seti ya rangi aina 10 , viatu Sh300 na brashi Sh100,” anasema.

Ngigi basi huuza viatu kati ya Sh550 hadi Sh700 kulingana na ugumu wa muundo. Wengi wa wateja wake ni wanawake lakini yeye vilevile hutengeneza viatu vya kiume na vya watoto.

Viatu alivyorembesha msanii Westbury Ngigi, 21. Picha/ Margaret Maina

Msanii huyu ameuza zaidi ya jozi 150 tangu Septemba 2019 na anatarajia kuitumia faida yake kutoka kwa mauzo kuanzisha studio ya kazi za sanaa.

Ufikiaji mkubwa wa uuzaji kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii na hamu inayokua miongoni mwa wateja wake vimesababisha kufanikiwa kwa Ngigi kibiashara kote nchini.

Mbali na kubadili mwonekano wa viatu Ngigi pia anachakata chupa za glasi na kuzibadilisha kuwa vipande vya mapambo kwa kutumia vitambaa vya Ankara.

Anapoulizwa kwa nini alianza kuchakata chupa za glasi, anasema kuwa hitaji la utunzaji wa mazingira lilimchochea.

“Niliona haja ya kuhifadhi mazingira na nilitafakari ni jinsi gani ninavyoweza kuzitumia vizuri chupa ambazo mara nyingi zinakuwa zimewekwa kila mahali kwa kuzisindika tena. Kwa hivyo, nilianza kuchakata kwa kuzibadilisha kuwa vipande vya sanaa,” anasema.

Kijana huyu anatarajia kupanua biashara yake na kutoa mafunzo kwa vijana wengine kwenye ustadi huo.

Anashauri vijana wasilalamike juu ya ukosefu wa kazi bali watumie talanta zao na ubunifu kujikimu kimaisha.

 

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Alama ya kistari kifupi, ritifaa...

RIZIKI: Uchoraji wamvunia donge na kumpa tonge

adminleo