Miroslav Klose ateuliwa kocha msaidizi wa Bayern Munich
Na CHRIS ADUNGO
MFUNGAJI bora wa muda wote katika timu ya taifa ya Ujerumani, Miroslav Klose, ameteuliwa kuwa kocha msaidizi wa kikosi cha Bayern Munich kwa minajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Bundesliga.
Klose, 41, amekuwa mkufunzi wa chipukizi wa Bayern kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita tangu aangike rasmi daluga zake katika ulingo wa soka mnamo 2016.
Mvamizi huyo matata aliwahi kuchezea Bayern kwa misimu minne kuanzia 2007 na kunyanyulia miamba hao wa soka ya Ujerumani mataji Bundesliga na makombe ya haiba katika mapambano mengine ya ndani kwa ndani.
“Hii ni hatua kubwa sana katika taaluma yangu ya ukocha,” akasema Klose ambaye kwa sasa atashirikiana na mkufunzi mkuu wa Bayern, Hansi Flick.
Flick ambaye alirefusha muda wa kuhudumu kwake kambini mwa Bayern mwezi uliopita wa Aprili 2020, alikuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Ujerumani wakati Klose alipokuwa sehemu ya kikosi kilichoshindia nchi hiyo ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil.
“Nimefahamiana vizuri zaidi na Flick tangu alipokuwa akinipokeza malezi ya soka ndani ya timu ya taifa. Tunaaminiana sana kitaaluma na katika maisha ya kawaida nje ya ulingo wa soka,” akasema Klose.
Klose alifungia Ujerumani jumla ya mabao 71 kutokana na mechi 137 alizosakatia timu hiyo ya taifa kati ya 2001 na 2014.
Mbali na Bayern, amewahi pia kuchezea vikosi vya Kaiserslautern na Werder Bremen nchini Ujerumani na Lazio ambayo kwa sasa inashiriki Ligi Kuu ya soka nchini Italia (Serie A).
Flick, 55, alitia saini mkataba mpya na Bayern mwanzoni mwa Aprili katika makubaliano ambayo kwa sasa yatamdumisha ugani Allianz Arena hadi mwisho wa 2023.
Kocha huyo alijiunga na Bayern mwanzoni mwa msimu huu akiwa msaidizi wa mkufunzi Niko Kovac aliyefurushwa mnamo Novemba 2019 kutokana na msururu wa matokeo duni ya mabingwa hao watetezi wa kipute cha Bundesliga.
Tangu awaongoze Bayern katika kibarua chake cha kwanza mnamo Novemba 10, Flick ameshuhudia kikosi chake kikisajili ushindi katika mechi 18 kati ya 21 alizozisimamia. Huu ni ufanisi uliomchochea Mwenyekiti Karl-Heinz Rummenigge kuwa mwepesi wa kumpa kandarasi mpya ya miaka mitatu zaidi.
“Kikosi kizima kimefurahishwa na juhudi za Flick. Bayern inazidi kuimarika pakubwa chini ya ukufunzi wake na soka ambayo tumekuwa tukipiga tangu mwishoni mwa mwaka jana imekuwa safi na ya kuvutia sana. Haya ni mambo ambayo yanaonekana wazi kupitia ubora wa matokeo ya timu na wingi wa mashabiki ambao kwa sasa tunajivunia duniani kote,” akasema Rummenigge.