• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
KARIOBANGI: Baadhi ya wahasiriwa wajihusisha na vitendo vya uhalifu

KARIOBANGI: Baadhi ya wahasiriwa wajihusisha na vitendo vya uhalifu

Na GEOFFREY ANENE

HUKU wahasiriwa wengi wa ubomoaji makazi mtaa wa mabanda wa Kariobangi Sewage wakianza kujiandikisha ili wapokee chakula cha msaada kutoka kwa wahisani ili kujikimu kimaisha, baadhi wameanza kujihusisha na uhalifu.

Walioachwa bila makao baada ya mtaa huo kubomolewa juma hili, sasa wamegeukia uhalifu na misaada ya chakula .

Mwandishi huyu alipozuru barabara ya Komorock Road mnamo Ijumaa, alishuhudia baadhi ya vijana wa kiume wakisimamisha magari ya watu binafsi, kuwasumbua na hata kuwaibia.

Kabla ya kuzuia barabara hiyo, vijana hao walisikika wakisema lazima waendelee na maandamano dhidi ya kufurushwa kutoka mtaani Kariobangi Sewage.

Walijikusanya kwa karibu kundi la kati ya watu 20 na 30 kwenye eneo lililokuwa na makazi ya Kariobangi Sewage, ambalo sasa limegeuka kuwa uwanja uliojaa taka ya kila aina baada ya mabuldoza ya serikali kubomoa nyumba zilizokuweko.

Barabara ya Komorock Road ilitumiwa kama lango kubwa la kuingia Kariobangi Sewage. Bado pia linatumiwa na wafanyabiashara na wanunuzi wanaoingia soko la Korogocho, ambalo pia upande mmoja uliokuwa umeshikana na Kariobani Sewage ulibomolewa.

Polisi, ambao walikuwa wamevalia kama raia, walifyatulia waandamanaji hao vitoamachozi na pia risasi ili kuwatawanya. Mmoja wa vijana hao alipigwa risasi tumboni na kupelekwa hospitali baada ya karibu dakika 20.

Mara kadha, vijana hao walikusanyika na kutawanywa tena na maafisa wa usalama, ambao waliamua kupiga doria kwenye barabara hiyo wakitumia lori lao.

Baada ya hali kutulia kidogo, mwandishi huyu alivuka barabara hiyo na kuingia kulikokuwa mtaa wa Kariobangi Sewage na kupata makundi ya watu waliojiita waathiriwa wa ubomoaji wa mtaa huo, wakijiandikisha majina na shirika moja lisilo la serikali.

Walihitajika kuwa na vitambulisho na kuthibitisha kuwa walikuwa wakiishi katika mtaa huo kabla ya kufurushwa.

Mtaa wa Kariobangi Sewage na sehemu ya soko la Korogocho iliyobomolewa ilikuwa imeziba mtaro wa kupitisha majitaka.

Waathiriwa wa ubomoaji huo waliandikisha majina yao ili wapokee misaada ya chakula kutoka shirika hilo.

Baadhi ya watu waliokuwa wakiandika majina kupokea misaada hiyo waliamini kuwa kuna watu ambao hawakufaa kupata misaada hiyo na walisikika wakitoa vitisho.

Foleni ndefu zilishuhudiwa bila ya wakazi kuwa mbali mita 1.5 baina yao kama inavyohitajika katika vita dhidi ya maambukizi ya virusi hatari vya corona. Wengi pia hawakuwa wamevalia barakoa.

Vuta n’kuvute kati ya serikali iliyobomoa eneo hilo na waliokuwa wakazi bado inatarajiwa kuendelea kwa muda usiojulikana, ingawa tayari wengi waliokuwa wakazi wa Kariobangi Sewage wamehamia kwingineko.

Baadhi yao walikuwa wamekesha siku kadha wakisema hawana pa kuenda.

Serikali inasema wakazi hao walitapeliwa kununua ardhi katika sehemu hiyo nao wakazi wanasema walinunua shamba hilo kwa njia halali mwaka 1996.

Mahakama ilikuwa imesimamisha ubomoaji wa makazi hayo, lakini serikali ilipuuza agizo hilo ikisema ardhi hiyo ni mali ya kampuni ya kusambaza maji na kusafisha majitaka ya Nairobi Water & Sewerage Company.

You can share this post!

Yaya Toure ampigia upatu Didier Drogba awe Rais mpya wa...

Serikali yasitisha ubomoaji zaidi Kariobangi

adminleo