Habari Mseto

Ichung’wah asema Rais astahili kuangazia zaidi changamoto zinazowakumba raia

May 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Kikuyu Kimani Ichung’wah (Jubilee) amesema Jumatatu serikali inapaswa kushughulikia Wakenya kikamilifu wakati huu wanakabiliwa na majanga.

Kauli yake inajiri saa chache baada ya mabadiliko ya hivi punde ya uongozi wa bunge la seneti chini ya chama tawala cha Jubilee.

“Tunajishughulisha kwa mambo yasiyofaa. Zaidi ya watu 200 wamekufa maji kutokana na mafuriko yanayoshuhudiwa sehemu tofauti nchini. Maelfu wameachwa bila makao Korogocho na maeneo yanayonyesha mvua kubwa,” amesema mbunge huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya bajeti katika bunge la kitaifa.

Amesema haoni juhudi za kisawasawa za wanasiasa kuangazia janga la Covid-19, mafuriko na kilio cha wananchi kukosa chakula kufuatia athari za corona.

“Rais Uhuru Kenyatta ahakikishe Wakenya wanapata chakula na aimarishe uchumi ambao umezoroteshwa na athari za Covid-19,” Ichung’wah akasema.

Kauli ya mbunge huyo imejiri kufuatia mkutano uliofanyika katika Ikulu ya Rais jijini Nairobi mapema Jumatatu, na ulioshirikisha maseneta wanaomuunga mkono Rais Kenyatta ambapo imefichuka ulilenga kuwang’atua viongozi wa Jubilee katika Bunge la Seneti wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ unaounga mkono Naibu Rais William Ruto.

Katika mkutano huo, seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, rafiki na mashirika wa karibu wa Dkt Ruto na ambaye amekuwa ni kiongozi wa wengi seneti ametemwa na nafasi yake akachukua Samuel Poghisio, seneta wa Pokot Magharibi (Kanu).

Seneta wa Nakuru Susan Kihika, mshirika mwingine wa karibu wa Naibu Rais na ambaye alikuwa kiranja wa seneti ameng’atuliwa, nafasi yake ikachukuliwa na Irungu Kang’ata (Murang’a).

Kulingana na Kimani Ichung’wah, mabadiliko hayo yamechochewa na ubinafsi katika uongozi.

“Huo ni mchakato wa tamaa ya uongozi kujitajirisha na unaochochewa na siasa zisizoheshimu demokrasia,” mbunge huyo akasema.

Naibu wa Rais Dkt William Ruto hakuhudhuria mkutano huo katika Ikulu.