Vijana wa Makongeni mjini Thika wataka serikali iwajali
Na LAWRENCE ONGARO
VIJANA kutoka Makongeni mjini Thika, wanalalamika kuwa mpango wa kuajiri vijana wasio na kazi haujawafikia hadi sasa.
Vijana hao walishangaa ni mbinu ipi ilitumika kuajiri vijana 1,500 hivi majuzi katika Kaunti ya Kiambu.
Kiongozi wa vijana eneo la Makongeni Bw Philip Mwenda alisema wamekuwa wakiona vijana kadha wakifanya kazi za mikoni katika mitaa tofauti lakini hawajaelewa jinsi walivyoajiriwa.
“Sisi hapa Makongeni tunazidi kupambana na shida na hatuna njia yoyote ya kujikimu. Tungetaka serikali kupitia afisi ya naibu kamishna Bw Douglas Mutai, ituangazie ili nasi tupate angalau kibarua cha kutupa mkate wa kila siku,” alisema Bw Mwenda.
Alisema tangu homa ya corona ilipofika hapa nchini, wao kama vijana wamekosa hata vibarua walivyozoea kufanya.
Mkazi wa Makongeni mjini Thika, Bw Benson Njoroge, alisema wengi wao wamekosa pesa za kulipa kodi za nyumba.
“Malandilodi hawatuonei huruma kwani wao wanataka walipwe pesa za nyumba bila kujali hali ya maisha ilivyo,” alisema Bw Njoroge.
Alisema vijana wengi wamekosa mwelekeo ambapo sasa wameweka matumaini yao kwa serikali ili iwaokoe.
“Hapa mitaani tumebaki wapweke; twaomba usaidizi haraka iwezekanavyo. Mara nyingine ukifika Makongeni utapata vijana wameketi bure bila kufanya lolote,” alisema Bw Njoroge.
Naye Bi Catherine Wanjiru alisema wamekumbwa na shida kuwa kwa sababu hata chakula cha kila siku hakipatikani kwa urahisi.
“Iwapo tutatafutiwa angalau chochote cha kufanya tutashukuru. Hatutabagua kazi yoyote,” alisema Bi Wanjiru.
Vijana hao walitaka maslahi yao yaangaliwe haraka iwezekanavyo kwa sababu walisema wanazidi kuteseka.
Naibu kamishna Bw Douglas Mutai alisema kulingana na mpango huo wa kuajiri vijana kazi eneo la Thika Magharibi liliteua vijiji vya Kiandutu na Kiang’ombe, ambavyo ndivyo vina idadi kubwa ya wakazi.
“Maeneo hayo mawili yana zaidi ya wakazi 35,000 na ndiposa yakawekewa zingatio. Hata hivyo, bado vijana hao wa Makongeni hawajasahauliwa,” alisema Bw Mutai.
Vijana wapatao 1,500 waliajiriwa wiki mbili zilizopita kama njia mojawapo ya kutii agizo la Rais Uhuru Kenyatta.
Kulingana na mpango uliopo, vijana hao watakuwa wakifyeka mitaa tofauti mjini Thika, na kuzibua mitaro hya majitaka maeneo tofauti huku wakilipwa Sh600 kila siku.