Michezo

Klabu za EPL kurejesha mabilioni kwa wapeperushaji wa mechi zao redioni na katika runinga

May 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

KLABU za Ligi Kuu ya Uingereza zinatarajiwa kurejesha jumla ya Sh47 bilioni kwa kampuni za upeperushaji mechi zao za kitaifa na kimataifa hata kama michuano tisa iliyosalia msimu huu itasakatiwa ndani ya viwanja vitupu bila mashabiki.

Vikosi vyote 20 vya EPL vilionywa kwamba huenda kiasi hicho cha fedha kikaongezeka hata zaidi iwapo msimu huu mzima utafutiliwa mbali au pasiwepo kikosi chochote kitakachoshushwa ngazi katika kampeni za muhula huu.

Vinara wa klabu zote husika za EPL walikutana Mei 11, 2020 kuzungumzia uwezekano wa kurejelewa kwa mechi 92 za msimu huu huku masuala kuhusu mipangilio ya kutoruhusu kikosi chochote kucheza katika uwanja wake wa nyumbani yakizamiwa zaidi.

Kurejeshwa kwa fedha ambazo awali zilikuwa za matangazo kutokana na kuonyeshwa kwa mechi moja kwa moja runingani ni suala lililopendekezwa na kikao hicho kwa kuwa mpangilio mzima wa msimu huu umevurugika: mechi zitapigiwa ndani ya viwanja visivyo na mashabiki na katika nyakati tofauti na jinsi ilivyoratibiwa mwanzoni mwa msimu huu.

Isitoshe, wasimamizi wa klabu zote husika za EPL wameombwa kufanikisha mipango ya kurejesha fedha za baadhi ya mashabiki waliokuwa wamelipia ada za kutazama mechi zote za vikosi vyao muhula huu.

Awali, Richard Masters ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa EPL alikuwa amekadiria hasara ambayo ingepata vikosi vya soka ya Uingereza kufikia Sh140 bilioni iwapo msimu huu ungefutiliwa mbali na pasiwpo mshindi wala vikosi vya kuteremshwa ngazi hadi Ligi ya Daraja ya Kwanza (Championship).

“Tulifanikiwa kuwapa wasimamizi wa klabu zote habari muhimu kuhusu hali ilivyo kati yetu na watangazaji. Siwezi kufichua yote tuliyojadili kwa sababu vikosi vyote havijaathiriwa kwa kiwango sawa,” akasema Masters.

“Hata iwe namna gani, hatimaye klabu zote zitakadiria hasara kubwa msimu huu. Hilo ni suala ambalo haliwezi kuepukika kwa sasa,” akaongeza.

Mwaka huu pekee, klabu zote za EPL zilizotia mkataba wa miaka mitatu na mashirika mbalimbali ya habari mnamo Agosti 2019, zilitazamiwa kuvuna jumla ya Sh126 bilioni kutokana na matangazo ya kibiashara kupitia vituo vya Sky Sport, BT Sport, Amazon, BBC na talkSPORT.

Fedha hizi zilitarajiwa kutokana na mechi katika mapambano ya League Cup, Kombe la FA, EPL, Europa League na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Japo kuna matarajio ya kurejelewa kwa kampeni za EPL mnamo Juni 12, bado hakuna maafikiano miongoni mwa washikadau.

“Baadhi ya wachezaji wana virusi vya corona na wanahofia unyanyapaa. Wengine waliwahi kusikia jinsi wenzao walivyougua na wanaogopa kutagusana nao kwa haraka. Wapo pia wachezaji ambao jamaa zao wana ugonjwa huu na haitakuwa vyema kuwalazimisha kurejea kambini wakati ambapo wapendwa wao wanawahitaji zaidi,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Watford, Scott Duxbury.

Awali, fowadi Sergio Aguero wa Manchester City alikuwa ameshikilia kwamba wachezaji ‘wanahofia’ kurejea uwanjani kusakata mpira wakati huu ambapo janga la corona bado halijadhibitiwa vilivyo.

“Wachezaji wengi wanasema kuna watu walio na virusi vya corona ila hawaonyeshi dalili zozote za ugonjwa huo. Itakuwa rahisi sana kwa watu kuambukizana iwapo hali itakuwa hivyo,” akasema mvamizi huyo wa timu ya taifa ya Argentina.

Vinara wa vikosi vya EPL na wasimamizi wa ligi hiyo wanapanga tena kukutana baadaye wiki hii kujadili suala la iwapo mikataba ya baadhi ya wachezaji iliyokuwa itamatike mwishoni mwa Juni itarefushwa na klabu husika hadi kampeni zote za msimu huu zitamatike rasmi.

TAREHE MUHIMU KATIKA SOKA YA EPL:

Jumatano, Mei 13: Chama cha Wachezaji na Chama cha Makocha wa vikosi vya EPL kushauriana serikali kuhusu mikakati na taratibu mpya za afya.

Alhamisi, Mei 14: Mikutano kati ya vinara wa Chama cha Wachezaji na Chama cha Makocha kujadili taratibu za afya zitakazokuwa zimetolewa na serikali.

Alhamisi, Mei 14: Mkutano kati ya Katibu wa Utamaduni na vinara wa soka ya EPL.

Jumatatu, Mei 18: Mkutano wa vikosi vyote vya EPL.

Jumatatu, Mei 18: Wachezaji wa EPL kurejea kambini mwa minajili ya mazoezi wakiwa makundini huku wakizingatia kanuni zote za afya zilizowekwa.

Jumatatu, Mei 25: Makataa ya wasimamizi wa soka ya bara Ulaya (Uefa) kuhusu mipango ya kukamilishwa kwa ligi kuu za bara Ulaya msimu huu.

Jumatatu, Juni 1: Serikali kutoa taarifa ya mwisho kuhusu tarehe mwafaka zaidi ya kurejelewa kwa baadhi ya michezo bila ya mahudhurio ya mashabiki au kutolewa kwa taarifa rasmi ya kufutiliwa mbali kwa msimu huu mzima na kufichuliwa kwa yatokanayo na maamuzi hayo.

Ijumaa, Juni 12: Kurejelewa kwa kipute cha EPL huku mchuano wa kwanza ukitandazwa bila mashabiki.