• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
UBUNIFU: Sanaa ya mosaic yawafaa pakubwa Daniel na Gladys

UBUNIFU: Sanaa ya mosaic yawafaa pakubwa Daniel na Gladys

Na MARGARET MAINA

[email protected]

SANAA ya mosaic inahusisha kuunganisha vitu kama manyoya, plastiki, nyasi, vipande vya vyuma au glasi kwa kutumia udongo au simiti na kupaka rangi tofautitofauti ambapo matokeo yanakuwa ni umbo la kuvutia ajabu!

Hii sasa imekuwa ni kazi ambayo wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Egerton, Nakuru, wanaitegemea sana.

Daniel Oguti, 22, na Gladys Anyika, 20, wote wakiwa wanasomea taaluma ya uchunguzi wa jinai na usalama, wanatengeneza bidhaa kwa kutumia ujuzi walio nao wa sanaa hii ya mosaic na kuuzia wateja na hivyo kuweza si tu kujilipia karo, bali pia kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Harakati zao za kujipa kipato na mapenzi yao kwa sanaa hii, vimeunganisha na kuwafanya marafiki wa kufa kuzikana Daniel na Gladys ambao wamelelewa Busia na Mathare mtawalia.

Akiwa na umri mdogo, Daniel alipenda sana kuchora na akiwa kidato cha pili, aliamua kujitosa katika sanaa hii ya mosaic akitumia vipande vya turubai, gluu na nyasi aina ya ‘olenge’ inayopatikana kwa wingi katika kaunti ya Busia.

Alianza kuuza na kutumia pesa alizopata kujilipia karo. Alifuzu mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) kwa kujizolea alama B+ na kujikatia fursa ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Egerton.

Kwa sasa akiwa ni mwanafunzi wa Mwaka wa Nne chuoni humo, akisomea taaluma ya jinai na usalama, anasema changamoto za kifedha alizoziona zimempanulia kinywa; tena chenye meno hatari, zilimfanya ajue kujitegemea na kutia bidii maishani.

Daniel ni mkubwa baina ya nduguze katika familia ya watoto wanne na alilelewa na babu yake. Sanaa hii ilileta nuru katika familia ambapo sasa aliweza kuisaidia pamoja na kuweza kujilipia karo. Kazi ya Mungu hiyo!

Amewauzia viongozi wengi baadhi ya bidhaa na mapambo anayotengeneza, bei ya chini ikiwa ni Sh1,500 kutegemea saizi, na huzitangaza kwa kutembea mlango hadi mlango.

Kazi nzuri ya sanaa ya mosaic ikionyesha mandhari ya Pwani. Picha/ Margaret Maina

Mambo si tofauti sana kwa Gladys kwani naye pia anasema wazazi wake walipata ugumu kumlipia karo pamoja na nduguze. Mwanadada huyu alipata alama ya B katika KCSE na mara alipojiunga na Chuo Kikuu cha Egerton, nyota ya jaha ilimkutanisha na Daniel, akawa mwanafunzi mzuri wa sanaa hii chini ya ushauri wa mzawa huyo wa Busia.

“Wazazi wangu walipata ugumu sana kunilipia mimi na ndugu zangu karo. Nilipojiunga na Chuo Kikuu nilijiambia kwamba nisingekubali upotovu wa maadili ambao umeshamiri katika taasisi za elimu ya juu uchukue udhibiti wa maisha yangu mara yakaja yakavurugika. Nilitaka nijishughulishe na kitu ambacho kingenipa kiasi fulani cha pesa; nisiwe mara ninawaambia wazazi nataka hiki, nataka kile. Kwa kweli ninaweza kusema sanaa hii ya mosaic imekuwa ya manufaa kwangu,” asema Gladys.

Daniel na Gladys hugawana faida baina yao ambapo hawakosi hata Sh20,000 au Sh30,000 kwa mwezi. Huu ni uchacharikaji ambao unashinda kubweteka tu pasi na kufanya chochote cha maana.

Kwa sasa wanalenga kujiimarishia hitaji lao la soko ili wauze bidhaa zaidi licha ya kwamba wana muda finyu zaidi wa kutangaza na kuchuuza bidhaa wanazotengeneza, huku wakihatajika kuhudhuria vikao vya darasa chuoni.

Kazi nzuri ya sanaa ya mosaic. Picha/ Margaret Maina

Ni kazi gani isiyo na changamoto? Kwa hawa wawili, wanalazimika kuchupa visiki kadha. Daniel analazimika kusafiri kwenda nyumbani Busia mara kwa mara kusudi apate nyasi aina ya olenge ambayo ni malighafi muhimu kwa kazi hii yake.

Wawili hawa wakati wanatembeza bidhaa zao wanagundua kwamba si watu wengi nchini ambao wametambua umuhimu wa sanaa kama hii yao. Hata hivyo, wanatarajia watu wataanza kutambua kazi zao.

Kwa sasa wawili hawa wanatamani wapate mdhamini wa kuwasaidia kufaulisha mpango wao wa kuwa na duka la kuweka bidhaa hizi kwa ajili ya kuzionyesha na kuuzia wateja pamoja na kufunza watu wanaotaka kuzamia kwa kazi hii ili nao wajue jinsi riziki inavyotafutwa bila kumpiga yeyote kabari.

Wanaona hii ni njia nzuri ya kuwapa vijana tumaini na kuwaepushia kadhia na kero ya mihadarati, ubwete, na kuwaepusha dhidi ya kujiingiza kwa vitendo vya kihalifu.

Wamewavutia vijana kadhaa na siku ile Gladys alimtumia dadake mdogo, Marion Nyangweso, 15, kadi ya heri njema wakati akikaribia kufanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE 2018), ulikuwa ni mwanzo mpya kwa mdogo wake huyo.

Kadi yenyewe iliyotengenezwa kwa sanaa hii ya mosaic ilikuwa maridadi na ikawa ni tiketi na msukumo wa moja kwa moja kwake Marion kuamua kuwa na zingatio kwa sanaa hii. Akawa naye anataka kujifunza jinsi ambavyo anaweza kutengeneza kitu kizuri kama hicho.

Alipokamilisha mtihani wake basi akahamia Nakuru kujiunga na Gladys.

“Nimeamua kufuata nyayo za dadangu kusomea taaluma ya kukabiliana na jinai kwa sababu hali katika mitaa ya mabanda imenifunza vya kutosha. Huko ni kama kubatizwa kwa maji moto. Pia nataka nijifunze sanaa hii yake ili name niwe na kitega uchumi cha kando,” asema Marion.

Tayari ameanza kuuza bidhaa zake naye akijitafutia karo ya shule ya sekondari.

Kwake Gladys anaiona sanaa kama mbinu nzuri ya kuwasiliana kwa kuwa inaweza pia kupitisha ujumbe wenye uzito mkubwa katika jamii.

“Wakati mwingine sisi wasanii tunaweza kutumia kazi hii kupitisha ujumbe unaomhitaji mtu pengine kujenga mapenzi kwa kazi hii ndiposa aweze kupata ujumbe unaopitishwa. Aghalabu kila kazi ina hadithi au msukumo wa kuwepo kwa kazi yenyewe,” asema Gladys.

Ni kwa maana hiyo ambapo Daniel na Gladys wanawashauri vijana kutumia vyema muda wao ili kujijengea msingi bora wa maisha yao.

You can share this post!

Mkenya Wanjiru Karani ateuliwa kuhudumu katika chama cha...

Mahakama yaagiza mshukiwa wa pili katika mauaji ya...

adminleo