• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 1:13 PM
Nyota wa Spurs akashifu mipango ya kurejelewa EPL kabla ya Covid-19 kudhibitiwa kabisa duniani

Nyota wa Spurs akashifu mipango ya kurejelewa EPL kabla ya Covid-19 kudhibitiwa kabisa duniani

Na CHRIS ADUNGO

BEKI Danny Rose wa Tottenham Hotspur amekashifu na kupinga vikali mipango ya vinara wa soka nchini Uingereza kurejelea kivumbi cha Ligi Kuu ya taifa hilo kabla ya virusi vya homa kali ya corona kudhibitiwa kote duniani.

Maafisa wa klabu zote 20 za EPL walikutana mnamo Mei 11, 2020, kujadili uwezekano wa kurejelewa kwa kipute hicho ambacho kiliahirishwa mnamo Machi 13 wakati wowote kuanzia Juni 12, 2020.

Hadi kufikia Mei 11, 2020, zaidi ya watu 32,000 walikuwa wameaga dunia nchini Uingereza kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

“Soka haistahili hata kuzungumziwa kwa sasa hadi wakati ambapo idadi ya visa vya maambukizi itashuka kabisa. Maisha ya watu yamo hatarini,” akatangulia Rose, 29.

Mnamo Mei 12, 2020, Chama cha Wachezaji wa Soka Duniani (PFA) kilifichua kwamba kilikuwa kimepokea malalamishi mengi kutoka kwa wanasoka ambao wana “hoja nzito” zinazopania kupinga hatua ya kurejelewa kwa kampeni za msimu huu katika mataifa mbalimbali.

Mapema mno

Kwa upande wake, Sadiq Khan ambaye ni Meya wa London, Uingereza alisema kwamba ni “mapema sana” kuanza kujadili uwezekano wa kusakata soka katika jiji kuu la Uingereza wakati ambapo maelfu ya watu wamepoteza maisha huku idadi kubwa ya wakazi wakiugua.

“Mbona tuwe wabinafsi kiasi hicho, tusifikirie familia zilizoathiriwa na maisha ya wale ambao tutakuwa tukiwaweka katika hatari zaidi ya kuambukizwa “gonjwa hili la ajabu” kwa sababu ya tamaa?” akauliza Khan.

Awali, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson alikuwa amepiga marufuku kuandaliwa kwa shughuli zozote za michezo hata kama zitakosa mahudhurio ya mashabiki, hadi Juni 1, 2020.

Rose ambaye kwa sasa anachezea Newcastle United kwa mkopo kutoka Tottenham, alifunguka na kufichua kiwango cha kutoridhishwa kwake na mikakati iliyopo katika juhudi za kurejelewa kwa EPL.

Mwanzoni mwa Mei 2020, fowadi Sergio Aguero wa Manchester City nchini Uingereza, alisema kuwa wachezaji ‘wanahofia’ kurejea uwanjani kusakata mpira wakati huu.

Msimu huu wa EPL ulitarajiwa kuendelezwa mnamo Juni 8, hali ambayo ingehitaji wachezaji kurudi mazoezini kikamilifu kufikia Mei 18.

Hata hivyo, vinara wa kipute hicho walisogeza mbele tarehe ya kurejelewa kwa kivumbi cha EPL hadi Juni 12, 2020.

“Wachezaji wengi wanaogopa kurejea uwanjani kwa sababu wana watoto na familia ambazo zinawategemea pakubwa,” akasema Aguero, 31.

Akihojiwa na runinga ya El Chiringuito nchini Argentina, Aguero aliongeza: “Ninaogopa sana. Hata hivyo, niko hapa na mchumba wangu, kwa hivyo sitatagusana na watu wengi. Nimejitenga nyumbani na mchumba wangu ambaye nadhani, ndiye mtu wa pekee ninayeweza kumuambukiza iwapo nitapata virusi hivi uwanjani,” akasema nyota huyo wa zamani wa Atletico Madrid.

You can share this post!

Magufuli akosa mkutano wa njia ya video wa EAC kujadili...

Nalenga kuvunja dhana potovu ‘Wakenya hawana lao soka...

adminleo